Miaka mitatu vita vya Syria
16 Machi 2014Hapo tarehe 15 mwezi wa Machi mwaka 2011 wiki chache baada ya uasi wa umma uliowan'gowa madarakani madikteta nchini Tunisia na Misri maandamano ya kupinga serikali yalizuka katika mji wa kusini nchini Syria wa Daraa baada ya vijana kukamatwa kwa kuchora ukutani maandishi ya kupinga serikali.
Vijana walichora kwenye kuta maandishi "Wananchi wanataka kuangushwa kwa serikali " wakiendeleza hisia zilizojitokeza mahala kwengineko katika ulimwengu wa nchi za Kiarabu wa kile kilichokuja kujulikana kama Vuguvugu la Majira ya Machipuko katika Ulimwengu wa Nchi za Kiarabu.
Serikali ya Rais Bashar la Assad ilitumia nguvu kukabiliana na hali hiyo na watu wakaanza kupoteza maisha yao. Maandamano hayo yalizagaa na nguvu kubwa zaidi ikatumika kuzima sauti zenye kudai mabadiliko.
Upinzani wapamba moto
Maandamano hayo yalizidi kupamba moto kila baada ya sala ya Ijumaa na kuzimwa kwa kutumia nguvu,raia wakabeba silaha,wanajeshi wakaanza kuasi na uasi huo ukageuka kuwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe baada ya serikali kushambulia kwa mbomu mji wa kati wa Homs hapo mwezi wa Februari mwaka 2012.
Miaka miwili baada ya hapo vita hivyo vikaonekana kufikia hali ya mkwamo baadhi ya watu waliokata tamaa wakisema huenda vikaendelea kwa miaka 10 hadi 15.
Waasi hivi sasa wanapigana wenyewe kwa wenyewe wakati wapiganaji wa jihadi wa kundi la Al Qaeda wakitaka kutunisha misuli yao na kudhibiti eneo kubwa la Syria.
Serikali inashikilia maeneo yenye kukaliwa na wakaazi wengi na mkakati wa Assad ni kulinda Syria yenye manufaa kwao yaani eneo la mwambao,miji mikubwa kaskazini na kusini na barabara muhimu.
Vikosi vya serikali vyasonga mbele
Huko Allepo ambao ulikuwa mji mkuu wa kibiashara wa Syria,serikali imelikomboa eneo la magharibi mwa mji huo wakati ikisonga mbele kwenye vitongoji vya mashariki vinavyoshikiliwa na waasi na vimeuchukuwa na kuufunguwa tena uwanja wa ndege ulioko karibu.
Leo vikosi vya serikali vimefanya mashambulizi makubwa ya anga, mizinga na vifaru na kuingia kwenye mji wa Yabroud ngome kuu ya mwisho ya waasi ilioko kwenye mpaka wa Lebanon na Damascus kaskazini.
Upinzani wa Syria ambao kwa kiasi kikubwa unaishi uhamishoni na unaotambuliwa na mataifa ya magharibi unaotaraji kukomeshwa vita hivyo kwa njia ya mazungumzo, unapuuzwa na waasi walioko kwenye mstari wa mbele wa mapambano.
Lakini licha ya kugawanyika kwao,upinzani wote unasisitiza kwamba suluhisho lolote lile la kisiasa halina budi kumuweka kando Assad ,lakini msimamo huo umegonga ukuta mapema mwaka huu wakati pande mbili kwenye mzozo huo zilipokutana Geneva chini ya shinikizo kutoka kwa washirika wao tafauti.
Ni wiki hii tu kumwekuwepo gumzo kwenye ngazi za serikali kuhusu uchaguzi ambapo Assad anatarajiwa kuwania tena kipindi chengine na kushinda kwa kishindo.
Haki za binaadamu zakiukwa
Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikiwaelezea waasi kuwa ni magaidi wanaoungwa mkono na mataifa ya magharibi na kudai kwamba imeweza kuendelea kuwepo hadi leo kutokana na kuungwa mkono na wananchi walio wengi.
Mashirika ya haki za binaadamu yamekuwa yakiishutumu serikali kwa kuhusika na unyama mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwafunga watu magerezani kuwatesa maelfu ya watu na kudondosha kutoka angani kile kinachojulikana kama mabomu ya mapipa na kwamba imekuwa haichaguwi baina ya wapiganaji na raia wakati wa kufanya mashambulizi yao.
Waasi hususan kundi la wapiganaji wa jihadi la Dola ya Kiislamu la Iraq na Sham pia wameshutumiwa kwa kukiuka haki za binaadamu.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema vita hivyo vimewalazimisha zaidi ya watu milioni tisa kuzikimbia nyumba zao na kuwa ndio kundi kubwa kabisa la watu waliopotezewa makaazi yao duniani.
Zaidi ya Wasyria milioni 2.5 wamesajiliwa au wanasubiri kusajiliwa kama wakimbizi katika nchi jirani ikiwa ni ziada ya watu milioni 6.5 waliopotezewa makaazi ndani ya Syria kwenyewe.
Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/Reuters
Mhariri: Sudi Mnette