Miaka 75 ya shambulizi la Atomiki mjini Nagasaki
9 Agosti 2020Nagasaki ilishambuliwa kwa bomu la Atomiki, siku tatu baada ya mji wa Hiroshima kushambuliwa kwa bomu la nyuklia na kuifanya Japan kuwa taifa pekee ambalo lilipigwa na silaha za atomiki.
Manusura wa shambulizi hilo, ndugu na wageni wa kimataifa wamehudhuria sherehe za kumbukumbu mjini Nagasaki na kutoa wito wa amani duniani. Idadi ya wageni waliohudhuria tukio hilo imepunguzwa kufikia watu 500 ukilinganisha na wageni 5,900 waliohudhuria mwaka uliopita.
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amerejelea ahadi yake kwamba Japan itaongoza "juhudi za jumuiya ya kimataifa za kufikia ulimwengu usio na nyuklia". Meya wa Nagasaki Tomihisa Taue naye amesema kuwa "kitisho cha kweli cha silaha za nyuklia hakijawasilishwa kwa usawa ulimwenguni", licha ya miongo kadhaa ya juhudi na wahanga kusimulia kile walichopitia.
Katibu mkuu wa Umoja wa Kimataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake uliosomwa na msaidizi wake Izumi Nakamitsu, ameonya kwamba "matarajio ya silaha za nyuklia kutumika kwa makusudi, au kwa bahati mbaya ni hatari sana"
Manusura wasimulia
Terumi Tanaka ambaye sasa ana umri wa miaka 88, wakati shambulizi hilo likitokea alikuwa na umri wa miaka 13. Anakumbuka kila kitu kilivyokuwa cheupe akiongeza kuwa, "niliona watu wengi waliokuwa wameungua na kujeruhiwa wakiondolewa...wale waliokuwa wamefariki tayari katika shule ya msingi iliyogeuzwa kuwa malazi". Tanaka alilieleza shirika la habari la AFP katika mahojiano ya hivi karibuni ambapo alipoteza shangazi zake wawili.
Kumbukumbu ya miaka 75 inakuja wakati wasiwasi ukizidi kuongezeka juu ya kitisho cha nyuklia kutoka Korea Kaskazini na kuzidi kwa mivutano baina ya Marekani na China juu ya masuala kadhaa ikiwemo usalama na biashara.
Mashambulizi ya mwaka 1945
Marekani ilidondosha bomu la kwanza la nyuklia katika mji wa Hiroshima Agosti 6 mwaka 1945 na kuwaua watu 140,000. Idadi hiyo inajumuisha wale walionusurika mlipuko lakini wakafariki baadae.
Siku tatu baadae Marekani ikadondosha bomu jingine katika mji wa bandari wa Nagasaki na kuwaua watu 74,000. Siku sita baada ya mashambulizi hayo ya Marekani, Japan ilisalimu amri mnamo Agosti 15, 1945 na kuhitimisha vita vya pili vya dunia.
Marekani haijawahi kuomba msamaha kwa kupoteza maisha ya raia wasio na hatia kwenye mashambulizi ya nyuklia ambayo, wanahistoria wengi wa magharibi wanaamini yalikuwa ya lazima kuhitimisha vita na kuepuka uvamizi ambao ungekuwa wa gharama zaidi.
Vyanzo: AFP/DPA