1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 75 tangu kambi ya Auschwitz ilipokombolewa

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
27 Januari 2020

Watu walionusurika kifo kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz wamekutana tena kwenye kambi hiyo nchini Poland tangu illipokombolewa miaka 75 iliyopita.

https://p.dw.com/p/3WsL9
Bundeskanzlerin Merkel besucht KZ Auschwitz
Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Watu hao waliozeeka kiumri waliweka maua kandokando ya ukuta wa kambi ambapo wafungwa wengi waliuliwa na mafashisti wakati wa vita vikuu vya pili. Viongozi kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kujiunga na wazee hao kwa ajili ya kukumbuka kukombolewa kambi ya Auschwitz na majeshi ya kisoviet  miaka 75 iliyopita.

Hata hivyo hafla hiyo inafanyika katika muktadha wa wasiwasi juu ya kujitokeza tena kwa chuki dhidi ya Wayahudi duniani  kote. Ujerumani pia leo imekumbuka ukombozi wa kambi hiyo ya mauaji kwa shughuli mbalimbali.

Rais wa Ujerumani  Frank - Walter Steinmeier amekutana na watu watatu walionusurika kwenye kambi hiyo kwa ajili ya mazungumzo, Hermann Höllenreiter, Peter Gardosch na Pavel Tussig walikuwa wageni wa heshima kwenye kasri la rais la Bellevue mjini Berlin. Wazee hao wote walipelekwa kwenye kambi ya Auschwitz wakiwa watoto. Baada ya mkutano huo rais Steinmeier ameandamana na wahanga hao kwenda kwenye kambi ya Auschwitz-Birkenau iliyopo nchini Poland. 

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
Rais wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Reuters/Pool/A. Sultan

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anatarajiwa kuweka shada la maua na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kumbukumbu  juu ya mauaji hayo ya halaiki yaliyofanywa na manazi wa Ujerumani ambapo maalfu ya Wayahudi waliuliwa. Watu zaidi ya milioni moja waliuliwa, idadi kubwa wakiwa ni Wayahudi.

Baadae leo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki watatoa hotuba za kufungua tamasha la kuchangisha fedha zitakazokabidhiwa kwa wakfu wa Auschwitz-Birkenau. Hata hivyo Ujerumani inakumbuka miaka 75 tangu kukombolewa kwa kambi hiyo huku kukiwa na wasi wasi juu ya kuongezeka tena kwa chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.

Waziri wa mambo ya nje Heiko Maas  amewaambia waandishi habari mjini Berlin kwamba Ujerumani italiweka suala la kupambana na chuki dhidi ya wayahudi kuwa muhimu sana katika ajenda yake ya kisiasa wakati nchi hiyo inajitayarisha kushika usukani wa kuongoza shughuli za Umoja wa Ulaya kwa muda wa nusu mwaka na pia kuwa Rais wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa baadae mwaka huu.

Watu zaidi ya milioni 25 wameshaitembelea kambi ya Auschwitz tangu mwaka 1947 nchini Poland. Na sasa kila mwaka watu zaidi ya milioni mbili kutoka duniani kote wanaitembelea sehemu hiyo iliyoko kusini mwa Poland. 

Vyanzo: DPA/AP/p.dw.com/p/3Wqzp