Miaka 72 ya mauaji ya Holocaust
27 Januari 2017Bunge la Ujerumani Bundestag, lilipanga kuwa na hafla ya saa moja kuwakumbuka mamilioni ya wahanga wa utawala wa wanazi . Pia hafla kama hiyo, iliandaliwa na sehemu kubwa ya mabunge ya Mikoa ya Shirikisho . Wabunge wa bunge la Mkoa wa Bavaria wamelizuru baraza la Senete la bunge la Jamhuri ya Czech, mjini Prague na kuweka shada la maua mahala pa kumbukumbu katika mji wa Litomerice.
Kiasi ya watu 4,500 waliuwawa katika mji huo ulioko kaskazini mwa Prague, palipokuweko kambi ya wahanga ya Flossenbuerg katika mpaka wa Bavaria kuelekea Jamhuri ya Czech.
Sambamba na hayo wanakumbukwa wahanga wa mpango wa mauaji wa Hitler, ambapo walemavu na wagonjwa jumla ya watu 300,000 waliuawa, wakionekana kama watu wasio na maana katika jamii, wahanga ambao kwa muda mrefu walisahauliwa.
Zaidi ya watu 70,000 waliuwawa kwa gesi ya sumu katika maeneo sita yaliokuwa yakidhibitiwa na Ujerumani baina ya Januari 1940 na Agosti 1941.
Katika hafla ya leo bungeni mjini Berlin iliohudhuriwa pia na Kansela Angela Merkel, Spika wa bunge la Ujerumani, Norbert Lammmert, alisema mpango huo ulikuwa wa kwanza ambapo ilitumiwa gesi ya sumu kwa wale walioonekana hawana maana kuishi na kugeuka kuwa majaribio kuelekea mauaji ya kimbari - Holocaust dhidi ya Wayahudi.
Mnamo mwaka 1996 Rais wa Ujerumani wakati huo, Roman Herzog, alipendekeza Januari 27, siku ya kukombolewa kambi ya Auschwitz, kuwa siku ya Ujerumani kuwakumbuka wahanga wa utawala wa Wanazi na tangu wakati huo inafanyika kila mwaka.
Mwaka 2005 Umoja wa Mataifa, ukaitangaza Januari 27 kuwa Siku ya Kimataifa kuwakumbuka wahanga wa mauaji ya Kimbari ya Holocaust, wakati wa vita vikuu vya pili vya Dunia- siku a majeshi ya Urusi yalipoikomboa kambi ya mateso ya Auschwitz nchini Poland 1945.
Miongoni mwa Wayahudi milioni 6 waliouwawa, milioni moja walikufa katika kambi ya Auschwitz, wengi katika kumbi za gesi, sambamba na maelfu ya wengine wakiwemo Wapoland, watu wa jamii ya Waroma, pamoja na Warusi waliokamatwa kama wafungwa wa kivita.
Mwandishi. Mohammed Abdul-rahman, dpa, afp
Mhariri:Yusuf Saumu