1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Imetimia miaka 50 tangu kuuwawa Martin Luther King Jr

Sylvia Mwehozi
4 Aprili 2018

Ikiwa leo ni miaka 50 tangu  mauaji ya mwanaharakati wa haki za kiraia nchini Marekani  Martin Luther King Jr, maoni ya Wamarekani juu ya usawa wa rangi yamebaki katika mgawanyiko kwa kiwango kikubwa.

https://p.dw.com/p/2vSME
Martin Luther King 1966
Picha: AFP/GettyImages

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni uliofanywa na kituo cha utafiti wa mambo ya umma cha shirika la habari la Associeted Press AP-NORC, wengi wa Wamarekani weusi waliohojiwa wanasema hawajaona maendeleo makubwa kuelekea usawa katika maeneo muhimu ambayo harakati za haki za kiraia  zilitaka kuyashughulikia. Miongoni mwa mambo yanayogusiwa ni pamoja na ukatili wa polisi dhidi ya watu weusi, mfumo wa haki ya jinai, na haki ya kupiga kura.

Hotuba ya Luther ya mwaka 1963 ya "nina ndoto", iligusia ukatili wa polisi kama miongoni mwa masuala ambayo wanaharakati wa haki za kiraia walitaka kukabiliana nayo. Utafiti wa maoni unaonyesha kwamba zaidi ya watu 7 kati ya 10 miongoni mwa Wamarekani weusi wanafikiri kwamba pamepigwa hatua kidogo au hakuna kabisa maendeleo yoyote namna polisi wanavyowashughulikia weusi katika kipindi cha miaka 50.

Martin Luther King I have a dream Rede USA Washington D.C. 1963
Martin Luther King akitoa hotuba ya nina ndoto mwaka 1963Picha: AFP/Getty Images

Wakati wa mauaji ya Luther King, idadi ya magereza ya Marekani ilikuwa sehemu ndogo ya idadi ya sasa, na kiwango cha wafungwa cha wamarekani weusi ilikuwa mara tano zaidi ya kiwango cha wazungu.  Hadi kufikia mwishoni mwa miaka ya 90, kiwango cha wafungwa weusi kiliongezeka zaidi ya mara nane ya kiwango cha wazungu.

Na kuhusu suala la wapiga kura, katika hotuba yake ya mwaka 1957 iliyopewa jina la "tupe kura", Luther King alitaka usawa katika kupiga kura na kusisitiza umuhimu wa kushiriki katika maisha ya kiraia. Hii leo asilimia 63 ya wamarekani weusi na karibu asilimia 90 ya wazungu wanaonyesha kuwa kumepigwa maendeleo katika eneo hilo.

Alipouawa miaka 50 iliyopita, mchungaji Martin Luthr King Jr, alikuwa akifanyia kazi kampeni ya kuwaunganisha watu maskini wa kutoka asili tofauti ili kudai nyumba bora, kazi na elimu. Bernice King ni binti wa Martin Luther King hapa anazungumzia ikiwa yale aliyoyaamini baba yake yanatekelezwa hivi sasa. "Sidhani tulifanya kazi nzuri ya kukubali kweli mambo ambayo alizungumzia na sasa tuko katika wakati huo wa kuzingatia misingi ipi tunayoendelea nayo kama taifa na jinsi gani tutaweza kukabiliana na kile ambacho hatimaye hatukukishughulikia"

AP Iconic Images Martin Luther King mit Malcolm X
Martin Luther King akiwa na Malcolm XPicha: AP

Hivi sasa, viongozi wa asasi za kiraia wanafufua kampeni ya watu maskini kwa maandamano ya siku 40, kuketi na maandamano mengine ya amani. Waandaji wa kampeni hiyo walijadiliana kuhusu mipango yao huko Memphis usiku wa kuelekea maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Luther.

"Maandamano ya kwanza ya siku 40 sio ya mwisho, ni mwanzo tu", anasema mchungaji William Barber wa Carolina Kaskazini, mmoja ya wenye viti wa kampeni iliyofufuliwa upya.

Kuanzia Mei 14 wachungaji, wanachama wa vyama vya wafanyakazi na wanaharakati wengine watahudhuria matukio kwenye karibu majimbo 30, yanayolenga bunge na serikali. Kisha maandamano makubwa yamepangwa kufanyika mnamo Juni 23 mjini Washington, sawa na kile Luther alichokuwa akikiamini.

Mbali na kuhamasisha wapigakura, masuala kadhaa yatakayogusiwa katika kampeni hiyo ni umaskini, ubaguzi wa rangi na masuala ya mazingira.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman