Miaka 28 ya Muungano Magazetini
4 Oktoba 2018
Tunaanzia na muungano, miaka 28 baadae. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika: "Miaka 28 baadae bado kuna usemi: wamagharibi wanaojinata na wamashariki wanaolalama. Anaetokea katika majimbo matano ambayo hayawezi tena kuitwa mepya na kuja kutafuta kazi na kujenga maskani yake magharibi, anaweza kuandika kitabu kuhusu majivuno ya watu wamagharibi ambao misemo yao, mitazamo yao na dhana zao mtu anaweza kusema ni za kibaguzi. Na kinyume chake pia, wajerumani magharibi wengi wanawajua wa mashariki ambao zaidi ya miongo miwili baada ya muungano bado wanahisi" sio yote yalikuwa mabaya. Mwenye kuwasikia wote hao hana budi isipokuwa kutikisa kichwa."
Muhimu zaidi ni kuvumiliana na kuheshimiana
Ili kuondokana na hali hiyo gazeti la "Badische Zeitung" linashauri: "Watu wanabidi wakaribiane, wastahamiliane na kuheshimiana-kwa masilahi ya demokrasia, haki na kwa kuzingatia, kama alivyosema spika wa bunge Wolfang Schaüble "uzalendo unaoambatana na wakati."
Serikali kuu inaweza
Serikali kuu ya muungano imefanikiwa kufikia makubaliano kuhusu mada mbili muhimu; kuhusu namna ya kupunguza matumizi ya dizeli na pia kuhusu sheria ya uhamiaji. Makubaliano hayo yamepokelewa kwa namna tofauti na wahariri. Mhariri wa gazeti la "Stuttgarter Zeitung" anaandika: "Serikali kuu ya muunganao inataka kudhihirisha inaweza pia kuwajibika. Baada ya mivutano ya miezi iliyopita , hivi sasa wamebadilisha dira. Ni muhimu kwa mshikamano miongoni mwa jamii, kuona malumbano kuhusu sera ya wakimbizi yamemalizika. Ni hatua muhimu hiyo. Kwamba CSU kwa mshangao wa wengi imebadilisha msimamo wake kuhusu suala hilo, ni jambo linalotia moyo."
Hilo halisaidii lakini
Na hatimae gazeti la "Allgemeine Zeitung" linaandika: "Kweli eti, CDU/ CSU na SPD wamezungumzia kwa kina na kufanikiwa pia kufikia makubaliano katika masuala muhimu. Hizo ni habari nzuri, lakini hazitoshi kushawishi maoni ya wapiga kura. Wanunuzi wanahisi kwa mfano, makubaliano kuhusu matumizi ya Dizeli ni kiini macho tu na ni ushahidi wa jinsi wanasiasa wanavyoshindwa kukabiliana na visa vya udanganyifu vinavyofanywa na viwanda vya magari."
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/inlandspresse
Mhariri: daniel Gakuba