1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugaidi bado ni kitisho kikubwa duniani

30 Aprili 2021

Miaka 20 iliopita wapiganaji wa jihadi walishambulia kwa pamoja balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania, na kuanzia wakati huo Ugaidi umeendelea kukita mizizi Mashariki mwa Afrika.

https://p.dw.com/p/32htE
Bombenattentat auf US-Botschaft in Nairobi
Picha: picture-alliance/dpa

Ilikuwa tarehe 7 mwezi Agosti mwaka 1998, saa nne na nusu asubuhi, wakati wauaji wawili waliripua lori moja lililokuwa limejaa mabomu  mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Nairobi, nchini Kenya. Dakika tisa baadae bomu lengine likaripuka katika balozi nyengine ya Marekani mjini Dar es Salaam katika nchi jirani ya Tanzania.

Takriban watu 224 waliuwawa katika mashambulizi haya mawili yalioharibu kabisa balozi hizo za Marekani na kusababisha kuporomoka kwa nyumba zilizokuwa karibu.

Somalia al-Shabaab Kämpfer
Baadhi ya wanamgambo wa Al shabaabPicha: picture alliance/AP Photo/M. Sheikh Nor

"Mashambulizi katika balozi za Marekani mjini Nairobi na Dar es Salaam yaliwashitua wengi, Watanzania wengi na Wakenya hawakuelewa ni kitu gani kilichomsukuma mtu kufanya unyama kama huo," alisema Murithi Mutiga mtaalamu wa masuala ya usalama katika shirika la kimataifa la uangalizi wa migogoro alipokuwa anakumbuka siku ya tukio.

Matukio hayo ya mashambulizi hayakutarajiwa, sio tu kwa wakenya na Watanzania lakini kwa dunia nzima. Hapajawepo na waathiriwa wengi namna hiyo katika shambulio lililofanywa na mtandao wa magaidi wa Al Qaidi ambao hata walikuwa hawajulikanni wakati huo. Awali mashambulizi ya wanamgambo wa kiislamu yalikuwa sana yakifanyika katika vituo vya kijeshi. Lakini ghafla Osama Bin Laden na kundi lake wakajipatia umaarufu mkubwa kimataifa kutokana na matukio yao maovu. 

Mashambulizi ya mwaka 1998 yalianzisha vita vikali dhidi ya Ugaidi

Wataalamu wengi wanasema mashambulizi yao yalianzisha mwanzo wa vita dhidi ya ugaidi, kufuatia Marekani kujibu mashambulizi hayo kwa kurusha makombora dhidi ya walengwa katika mataifa mbali mbali.

Japokuwa shambulizi lenyewe halikuwalenga waafrika lakini Afrika Mashariki pakawa mahala pa kwanza kundi hilo la kigaidi la al Qaeda lilipoanzisha shambulizi lake la kwanza na kusababisha watu wengi kupoteza maisha. Mutiga aliiambia DW kwamba Afrika imethibitika kuwa eneo rahisi kushambuliwa.

Kenia Mombasa Angriff auf Polizeistation
Polisi na raia wakiitizama miili ya wanawake wawili baada ya shambulizi la kigaidi mjini Mombasa mwezi Septemba mwaka 2016 Picha: picture-alliance/dpa

Wataalamu wengi walibashiri kwamba Afrika itakuwa eneo litakolokuwa sugu kwa mashambulizi ya kigaidi kwa siku za usoni kutokana na mataifa kutokuwa na mifumo imara ya kiusalama hasa katika eneo linalokumbwa na vita la Somalia, linaloweza kutoa hifadhi kwa magaidi na kuwasajili wapiganaji wepya.

"Nadhani lile lililohofiwa ndilo lililopo," alisema Annette Weber, mtaalamu wa Afrika Mashariki, katika taasisi ya kijerumani ya masuala ya kimataifa na usalama.

Wanamgambo wa Al-shabab walio na mafungamano na kundi la kigaidi la al qaeda wanaendelea kushambulia. Lakini fikra ya kwamba ugaidi wa karne hii ya 21 utakita mizizi tu katika bara la Afrika sio ya kweli, ni wazi kwamba maeneo yanayolengwa zaidi ni Mashariki ya Kati. 

Weber, ameongeza kuwa wahalifu wa sasa ni tofauti sana na wahalifu au magaidi waliokuwepo miaka 20 iliyopita. Badala ya makundi madogo ya kundi la al Qaeda yaliosafiri katika maeneo waliolenga ili kushambulia, sasa ni makundi makubwa yanayokusanyika na kuchanganyikana na jamii.

Huku hayo yakiarifiwa kwa wakati huu vita dhidi ya ugaidi vimegawika kwa utawala wa sheria na ugunduzi wa kijasusi. Mutiga anamalizia kwa kusema huwezi kujua shambulizi jengine litatokea lini lakini mashambulizi sasa yanaonekana kuwa ya kiwango cha chini kuliko ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.

Mwandishi: Amina Abubakar/DW Page

Mhariri: Gakuba, Daniel