1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgonjwa wa Ebola Scotland awasili London

30 Desemba 2014

Mtumishi wa kwanza katika sekta ya afya ambae amegundulika kuambukizwa virusi vya Ebola nchini Uingereza amewasili mjini London kwa matibabu.

https://p.dw.com/p/1EDNi
Ebola Patient London Großbritannien 30.12.
Picha: Reuters/Neil Hall

Mwanamke huyo alifikishwa katika hospitali iitwayo Royal Free, ambayo imetengwa mahususi kama kituo cha kukabilina na maradhi ya Ebola. Mwandishi habari wa shirika la habari la Uingereza Reuters alisema mgonjwa huyo alifikishwa kituoni hapo kwa gari la wagonjwa, likisindikizwa na magari mengine kadhaa ya polisi.

Paul Cosford, ambae ni mkurugenzi wa kinga katika chombo cha serikali kilichoundwa kushughulikia mripuko wa Ebola kinachoitwa Afya ya Jamii, alisema wanafikiri taratibu za kitabibu kwa mgonjwa huyo zinakwenda kama ilivyotarajiwa.

Akizungumza na kituo cha radio cha shirika la utangazaji la BBC alisema walifikia makubaliano ya kitaifa kwa hospitali ya Royal Free ndio mahala mahususi kwa tiba ya watu walioambukizwa Ebola kwa kuwa ina vifaa na wataalamu kwa ajili ya ugonjwa huo.

Shirika la Afya Duniani WHO hapo jana lilisema idadi ya watu walioambukizwa virus vya Ebola katika mataifa matatu yaliathiriwa zaidi huko Afrika Magharibi ambayo ni Sierra Leone, Liberia na Guinea imepindukia 20,000 huku idadi ya vifo ikiwa zaidi ya 7,842 mpaka sasa.

Sierra Leone Ebola
Kituo cha matibabu ya Ebola Sierra LeonePicha: REUTERS/Baz Ratner

Mfanyakazi huyo wa shirika la huduma za afya la Uingereza, ambae amekuwa akifanya kazi Afrika Magharibi, kupitia asasi ya kimataifa ya kuhudumia watoto ya Save the Children, aliondoka Jumapili Sierra Leone kwa kutumia ndege ya shirika la ndege la Uingereza British Airways, kupitia Casablanca nchini Morocco na hatimae kuwasili uwanja wa ndege wa Heathrow mjini London.

Alibainika kuwa kuwa na virus vya Ebola Jumatatu na kwa mara ya mwisho alikuwa akitibiwa katika hospitali moja inayoitwa Gartnavel huko Scotland.

Serikali ya Scotland ilisema ugonjwa huo ulibainika katika hatua za mwanzo kabisa, kwa maana ya kwamba hatari ya mambukizi kwa watu wengine inatazamwa kuwa ya kiwango cha chini sana, lakini wanachukua hatua zote za kuenea kwa virus hivyo.

Liberia Monrovia Zentrum Deutsches Rotes Kreuz
Kituo cha matibabu ya Ebola LiberiaPicha: DW/J. Kanubah

Mapema kabisa mwaka huu hospitali ya Royal Free ilifanikiwa kumtibu mgonjwa mwingine, William Pooley, ambae alirejea nyumbani kwa ajili ya matibabu baada ya kubainika akiwa na maambukizi ya virus vya Ebola huko Sierra Leone.

Waziri wa kwanza wa Scotland, Nicola Sturgeon alisema mgonjwa wa pili amefanyiwa vipimo vya virusi baada ya kurejea kutoka Afrika Magharibi. Ingawa kuna uwezekano mdogo wa kuwa na maambukizi ya virusi,hakuwa na muingiliano na watu walioathiriwa.

Na Idara ya afya ya umma nchini Uingerza imesema mtu mwingine wa tatu anaendelea kuchunguzwa huko Cornwall, Uingereza na anapatiwa matibabu katika kitengo maalumu, na matokeo yake yatataolewa katika kipindi cha masaa 24.

Mwandishi: Nyamiti Kayora RTR
Mhariri:Idd Ssesanga.