Mgogoro wa Syria upatiwe uvumbuzi-wachambuzi
8 Januari 2014Wachambuzi wanasema kuwa vita hivyo vigumu vinavyojumuisha muungano mkubwa wa waasi wanaopinga serikali ya Syria ambao pia wana matawi katika nchi jirani za Iraq katika vita dhidi ya Rais Bashar Al-Assad, na lazima vitafutiwe suluhu.
Wachambuzi hao wamesema kuwa kuna mchanganyiko wa sababu kutoka ndani na nje ya Syria, ambazo zinasababisha kuongezeka kwa vurugu dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Sham, ISIL, na makundi mengine, na hivyo kuchochea mgogoro wa vita, unaoendelea nchini Syria,
Mtaalamu wa masuala ya Usalafi, Romain Caillet, amesema uhusiano uliopo kati ya kundi hilo la wanamgambo na wapinzani wengine wamezidisha mapambano na kuendelea kuchochea vita dhidi ya serikali.
Mauaji, kuteswa na kutekwa ni changamoto
Kuendela kwa vita nchini Syria kunasababisha kushamiri kwa vitendo vya mauaji yakiwemo mauaji ya hivi karibuni ya daktari maarufu wa kundi la waasi, Abu Rayyan aliyehusishwa na kundi moja la kigaidi na lenye ngugu la Ahrar-al-Sham, ambaye alitekwa, kuteswa na baadaye kuuawa na wanamgambo wa kundi hilo lenye itikadi kali la ISIL.
Mauaji ya mateso dhidi ya kiongozi huyo na wanamgambo hao ni suala lililowashtua watu wengi katika Jimbo la Allepo, tukio lililoelezwa kuwa kubwa na hivyo kundi hilo kutupiwa lawama na viongozi wa waasi kutangaza rasmi vita dhidi ya makundi yenye itikadi kali.
Tabia za kundi hilo la wanamgambo wenye itikadi kali haivumiliki miongoni mwa makundi ya waasi, anasema Thomas Pierret, mchambuzi mwingine wa masuala ya Syria na kuongeza kuwa makundi mengi yalitaka kulitawala eneo la Kaskazini mwa Syria kwa muda mrefu, lakini yalizuiliwa na kundi la Ahrar-al Sham linaloshirikiana na kundi la wanamgambo la ISIL, ambayo ndiyo yamekuwa yakishikilia eneo hilo.
Waasi wapigana tofauti dhidi ya Assad
Makundi mengi yanayoaminika kuwa ni ya kigaidi nchini Syria yanaendeleza mapambano dhidi ya serikali ya Bahar-al Assad ambapo kundi la Al-Nusra lenye viongozi wengi ambao siyo raia wa Syria limekuwa likipigana tangu mwanzoni mwa mwaka 2012.
Mwezi Aprili mwaka jana kiongozi wa kundi la waasi la al-Qaida nchini Iraq, Abu-Bakr al-Baghdad, alitangaza rasmi kuwa kundi lake la AQI lilikuwa limeungana na kundi jengine la al-Nusra la ndani ya Syria.
Hata hivyo, al-Nusra ilikanusha kuungana na AQI, na sasa makundi hayo yanapigana tafauti kwenye uwanja wa mapambano dhidi ya utawala wa Assad.
Muungano wa makundi ya upinzani nchini humo, National Coalition, unayatuhumu makundi ya kigaidi kwa kudhoofisha mapinduzi dhidi ya Rais Bashar al-Assad.
Desemba mwaka jana, Marekani na Uingereza zilitangaza kufuata misaada yake kwa upinzani kwa kuhofia kuchochea mgogoro wa vita kutoka kwa makundi ya Kiislamu.
Huku hayo yakiarifiwa, mazungumzo ya amani kukomesha mgogoro wa Syria uliodumu kwa karibu miaka mitatu sasa na kuangamiza maisha ya watu wasiokuwa na hatia, unatarajiwa kuanza Januari 24, mwaka huu mjini Geneva.
Mwandishi: Flora Nzema/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef