Mgogoro wa Qatar na tafsiri ya ugaidi
7 Julai 2017Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Bahrain zimetoa orodha ya makundi 24 na watu binafsi karibu 60 wanaodai wamekuwa wakishiriki katika kufadhili ugaidi na wanahusiana na Qatar. Qatar inasisitiza inalaani ugaidi na kwamba haiungi mkono makundi ya itikadi kali.
Taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa nishati ya gesi ni mshirika muhimu wa Marekani katika kanda hiyo inayokumbwa na machafuko. Inao wanajeshi karibu 10,000 wa Marekani walioko katika kambi ya jeshi la anga inayotumiwa kufanya mashambulizi dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq.
Orodha iliyotolewa na majirani za Qatar inaakisi wasiwasi wa muda mrefu ulioelezwa na maafisa wa Marekani. Wakati huo inahusisha pia wale wanaotofautiana kisiasa na sauti za upinzani.
Akizungumza mjini London siku ya Jumatano, waziri wa mambo ya nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, alisema madai dhidi ya nchi yake yamesanifiwa kujenga hisia za chuki dhidi ya Qatar katika mataifa ya magharibi.
"Tunaamini suala kuu siyo kuhusu ugaidi, suala kuu ni tofauti zinazopingana na namna ya kunyamazisha sauti nyingine, na pengine wanaiangalia Qatar na wanadhani kwamba Qatar imefanikiwa zaidi kuliko wao," alisema waziri Al Thani.
Udugu wa Kiislamu mwiba wa kooni
Wakati wakizungumza mjini London, mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka mataifa manne ya Kiarabu walikuwa wanakutana Cairo kuangalia majibu ya Qatar kuhusu madai yao. Juu kabisa katika madai hayo ni kwa Qatar kusitisha kuliunga mkono kundi la Udugu wa Kiislamu, lililoshika madaraka kwa muda mfupi nchini Misri na ambalo makundi chipukizi yake yako mashughuli kote Mashariki ya Kati.
Ingawa Qatar imekandamiza wapinzani nyumbani kwake, inauona Udugu wa Kiislamu kama kundi halali la kisiasa. Msimamo huu umeiweka katika mfarakano na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri, ambazo zinauona Udugu wa Kiislamu kama kitisho kwa utulivu wa kisiasa na usalama.
Al Thani alisema kuna hatari katika kuwaita wapinzani wa kisiasa kuwa ni magaidi ili tu kuwanyamazisha. "Majirani zetu wanachukulia mabadiliko - wale wanaoyatetea na wanaoripoti juu yake kama kitisho, na wanakuwa wepesi kumuita yeyote anaepinga serikali zao gaidi.," alisema Al Thani.
Zamani mshirika, sasa gaidi
Kiongozi wa kiroho wa Udugu wa Kiislamu Sheikh Youssef al-Qaradawi, alikuwa miongoni mwa waliotuhumiwa na majirani za Qatar kwa kuwa na uhusiano na ugaidi. Al, Qardawi, raia wa Misri mwenye umri wa miaka 90, ambaye ameishi Qatar kwa miongo kadhaa, huko nyuma alikuwa akikubaliwa na viongozi wa mataifa ya Ghuba na kuchukuliwa katika nafasi sawa na Mufti mkuu wa Saudi Arabia Sheikh Abdelazizi Al Sheikh, na watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mwaka 2013, aliungana na wahubiri kadhaa wa Ghuba kuwataka vijana wawalinde Waislamu wa Kisunni nchini Syria, miito ambayo ilishabihiana na uugaji mkono rasmi wa waasi wanaopambana kumuondoa rais wa Syria Bashar al-Assad.
Al-Qardawi alitofautiana na wahubiri wa Ghuba alipoikosoa serikali ya Misri baada ya kuupindua Udugu wa Kiislamu kutoka madarakani. Aliyakosoa pia mataifa ya Ghuba yaliyounga mkono ukandamizaji wa kikatili dhidi ya wafuasi wa kundi hilo.
Hatua ya Qatar kuunga mkono Udugu wa Kiislamu imeifanya kutofuatiana na wenzake, kama ulivyokuwa mchango wake maalumu kama mpatanishi katika majadiliano ya kuachiwa mateka, ikisaidia kuwaachia huru mateka wa nchi za magharibi walioshikiliwa na Al-Qaida nchini Syria na Yemen.
Wafadhili wa ugaidi
Orodha iliotolewa na mataifa manne inataja majina ya raia wa Qatar wakiwemo Khalifa al-Subaie, Saad al-Kabi, Abdelrahman al-Nuaymi, Ibrahim al-Bakr na Abdel-Latif al-Kuwari. Wote wamewekewa vikwazo na wizara ya fedha ya Marekani kama wafadhili wa Al-Qaeda. Watano hao wanaonekana kuishi Qatar - mali zao zimezuwiwa, wako chini ya uchunguzi na wamepigwa marufuku kusafiri nje ya nchi - lakini hawajafungwa.
David Weinberg kutoka Wakfu wa ulinzi wa demokrasia, ambaye ameandika sana kuhusu ufadhili wa ugaidi katika eneo la Ghuba, anasema Qatar imefanya uzembe usiosameheka linapokuja suala la kukandamiza wafadhili hao wa makundi ya itakadi kali.
Weinberg anasema kumekuwepo na mjadala wa muda mrefu ndani ya serikali ya Marekani kuhusu iwapo msimamo laini wa Qatar unahusiana na kukosa uwezo au nia, na anasema utafiti wake unaonyesha kuwa ni kukosa nia.
Lakini pia yapo madai kama hayo kwa upande mwingine ambapo Saudi Arabia imetuhumiwa wiki hii na kundi moja la mrengo wa kulia nchini Uingereza kwa kutumia fedha nyingi kufadhili makundi ya itikadi kali. Hilo limezidisha shinikizo kwa serikali ya Uingereza kuweka wazi utafiti kuhusu mchango wa Saudi Arabia katika kuchochea itikadi kali nchini humo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape
Mhariri: Josephat Charo