China yakanusha madai ya Marekani kuwa inafanya ujasusi
23 Julai 2020Wizara hiyo pia imekanusha madai ya Marekani na kusema Washington inaisingizia China kuwa inafanya ujasusi wa kiuchumi nchini humo.
"Ombi la Marekani la kuitaka China ifunge ubalozi wake mjini Houston ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na kanuni za msingi za uhusiano wa kimataifa," amesema Wang Wenbin, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China.
Wenbin ameongeza kuwa hatua hiyo itavunja daraja la urafiki kati ya raia wa China na Marekani.
Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje wa China pia amekanusha madai kuwa ubalozi huo umekuwa ukifanya upelelezi wa uchumi wa Marekani.
Badala yake, Wenbin amesisitiza kuwa ubalozi huo umejitolea kukuza uhusiano na ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili kwa zaidi ya miaka 40 kwani ni ubalozi wa kwanza wa China kuwepo nchini Marekani baada ya uhusiano kati ya mataifa hayo mawili kurudi kama kawaida.
Beijing yaonya kuwa itajibu hatua za Marekani iwapo utawala wa Trump haitaondoa vikwazo dhidi ya raia wake
Jumatano 22.07.2020, China ilionya kuwa itajibu hatua za Marekani iwapo utawala wa Trump hautaondoa vikwazo ilivyoweka dhidi ya baadhi ya raia wa China ifikapo kesho Ijumaa.
Agizo la Marekani lilifuatia uamuzi wa idara ya sheria nchini humo kuishtaki China kwa kusaidia wadukuzi wawili waliolenga kampuni kubwa kubwa za teknolojia kwa muda mrefu. Wadukuzi hao wanadaiwa kupanga kuzishambulia kampuni hizo ambazo zilikuwa zinaifanyia utafiti chanjo ya ugonjwa wa Covid-19.
Juu ya hayo, Wenbin pia ameikosoa Marekani kwa kumshtaki mtafiti wa China Song Chen, anayedaiwa kuwa mwanachama wa jeshi la ukombozi la China (PLA) ambaye sasa anahudumu katika ubalozi wa China katika jimbo la San Francisco.
Waendesha mashtaka wa Marekani wanadai kuwa Song aliingia Marekani mnamo mwezi Novemba mwaka 2018 ili kufanya utafiti katika chuo kikuu cha Stanford japo alishindwa kuelezea mafungamano yake na jeshi hilo la PLA wakati alipokuwa akiomba cheti cha usafiri cha Visa.
Song ametiwa hatiani kwa kufanya udanganyifu katika maombi ya visa na pia kwa kutoa habari za uwongo kwa idara ya upelelezi ya Marekani ya FBI.
Mtafiti huyo amewaambia waandishi habari kuwa yeye ni muathirika tu wa msuguano kati ya China na Marekani.
Rais wa Marekani Donald Trump anafikiria kupiga marufuku wanachama wa chama cha Kikomunisti wakiwemo wasomi na hata wanafunzi kuingia nchini humo.
China imeweka sharti kuwa ni lazima mtu awe mwanachama wa chama cha Kikomunisti ili apate fursa ya masomo ama za kujiendeleza kikazi. Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali, China Daily, mnamo mwaka 2019 chama hicho kilikuwa na zaidi ya wanachama milioni 90.
Chanzo dpa