1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfuko wa Mandela wamtaka Zuma ajibadilishe

1 Novemba 2016

Mfuko wa Mandela umesema uongozi wa Rais Zuma unahatarisha demokrasia nchini humo, na umemtaka abadilisha njia zake za uongozi.

https://p.dw.com/p/2Rzg6
Südafrika Kapstadt Jacob Zuma Präsident
Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Mfuko wa hisani ulioanzishwa kulinda urithi wa marehemu, Nelson Mandela, unamlaumu Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, kwa kile inachokitaja kuwa ni "kupoteza muelekeo" wa taifa hilo la Afrika lililoendelea kiviwanda, na linamtaka abadilishe uongozi wake wa kisiasa.

Tokea kuingia madarakani mwaka 2009, Zuma ameweza kuziepuka kashfa kadhaa za rushwa bila ya majeraha yoyote. Lakini Afrika Kusini ililazimika kubeba gharama ya matendo yake, wakati wawekezaji wakiwa na wasiwasi juu ya utulivu wa kisiasa, mazingira ya kibiashara pamoja na utawala wa sheria.

Katika taarifa isiyo ya kawaida, mfuko usio wa kiserikali, ambao wanachama wa bodi yake ya uongozi ni wasomi kutoka Afrika Kusini, wanasiasa na waandishi habari, wamekitolea mwito chama tawala cha Zuma cha African National Congress (ANC) kifanye mabadiliko ya uongozi wake.

"Tunakitolewa mwito chama tawala kuchukua hatu zitakazo hakikisha uongozi wa taifa unalidwa na kuwekwa katika hali salama na katikamikono ya viongozi walio na uzowefu," imesema taarifa hiyo.

Zuma hana dalili ya kujiuzulu

Südafrika Proteste Studenten Universität
Maandamano ya wanafunzi wanaopinga ada kubwa ya vyuo vikuu Afrika KusiniPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

Zuma mwenye umri wa miaka 74, anakabiliana na miito inayomtaka ajiuzulu kutoka kwa wanachama kadhaa wa chama cha ANC tokea uchaguzi wa mitaa mwezi Agosti, ambapo chama hicho kilishindwa vibaya tokea kilipoingia madarakani baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi mwaka 1994. Hata hivyo, viongozi wa ngazi za juu bado wanaendelea kumuunga mkono Zuma.

Upinzani pamoja na asasi za kiraia wamepanga kuandamana katika mji wa Pretoria kesho kutwa Jumatano, kudai miongoni mwa mambo mengine kwamba Zuma ajiuzulu.

Lakini Zuma haoneshi dalili za kujiuzulu kabla ya kumaliza muhula wake wa mwisho kama rais mwaka 2019, licha ya kuzongwa na kashfa za rushwa ambazo zimemuumiza kifedha pamoja na kuchafua umaarufu wake wa kisiasa.

Mwezi Machi, Mahakama ya Katiba ilimuamuru kulipa dola milioni 16 alizozitumi kuratibu nyumba yake binafsi mjini Nkandla jimbo la KwaZulu-Natal. Lakini Zuma alinusurika na kura ya kutokuwa na imani naye bungeni kuhusu kashfa hiyo na hadi sasa ameshalipa kiasi cha dola 500,000.

Mfuko wa Mandela umesema amri ya mahakama kuhusu kesi hiyo ya Nkandla, ni mfano unaoonesha namna Zuma alivyoshindwa kuitekeleza katiba ya nchi.

Ongezeko la ukosefu wa ajira pamoja na kuporomoka kwa uchumi kunazidi kuupa jina baya uongozi wa Zuma. Serikali yake pia imeshindwa kuzima maandamano ya vurugu yanayofanywa na wanafunzi karibu kila wiki, juu ya gharama kubwa za elimu ya vyuo vikuu.

Taarifa hiyo ya mfuko wa kiongozi wa zamani wa Afrika Kuisni, Nelson Mandela, umesema umeshuhudia kudhoofika kwa utekelezaji wa sheria chini ya uongozi wa Zuma na unaunga mkono haja ya kuwawajibisha waliohusika kuiweka matatani demokrasia ya nchi pamoja na uporaji wa rasilimali zake.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri:Yusuf Saumu