Mfalme wa Uingereza akosolewa kwa kukimya juu ya machafuko
9 Agosti 2024Ingawa mfalme huyo na mkewe Camila walitoa salamu za rambirambi kwa familia za watoto hao watatu waliouawa Julai 29, kasri la Buckingham halijazungumza chochote kuhusu machafuko yaliofuatia tukio hilo.
Baadhi ya wadadisi wameeleza kushangazwa na ukimya huo wa Mfalme Charles, huku mtaalamu wa katiba akisema mfalme hazungumzii matukio hai ya kisiasa. Ameongeza kuwa wanatarajia familia ya kifalme kuzuru maeneo yaliokumbwa na machafuko baada ya hali kutulia.
Ukimya wa Charles unaelezwa kufuata nyayo za mama yake, hayati Malkia Elizabeth II, ambaye pia alisalia kimya wakati wa wimbi la machafuko nchini England mwaka 2011.
Maafisa wa serikali ya Uingereza wamelaumu machafuko hayo, ambayo yameshuhudia misikiti na vituo vya kuhifadhi wakimbizi na waomba hifadhi vikilengwa na wafuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia na majambazi, ambao wamewatuhumu kujaribu kutumia janga hilo la uchomaji kisu, pamoja na wasiwasi unaozidi wa mrengo mkali wa kulia kuhusu viwango vya uhamiaji, kufanikisha ajenda zao.