Mexico yashindwa kuchukuwa hatua vifo vya wanafunzi 43
1 Aprili 2023Kundi la wataalamu huru wa haki za binaadamu, The Interdisciplinary (GIEI), limesema kuwa mamlaka nchini Mexico zimeshindwa kutekeleza agizo la waendesha mashtaka la kukamatwa kwa waliohusika na kupotea kwa wanafunzi 43 mwaka 2014 huku jeshi likibana ufikiaji wa habari muhimu.
GIEI imeelezea wasiwasi kuhusu kuendelea kucheleweshwa kwa uchunguzi kuhusiana na kesi hiyo.
Soma zaidi: Wahamiaji 39 wafa kwa moto Mexico
GIEI, ambayo imekuwa likifuatilia uchunguzi huo, imelihimiza jeshi kushirikiana katika kutoa taarifa na kwa waendesha mashtaka kutoa maagizo zaidi ya kukamatwa kwa waliohusika.
Carlos Beristain, mjumbe wa GIEI, amesema kesi hiyo haiwezi kutatuliwa kwa kuzuia habari au kutoa majibu ambayo hayalingani na ukweli.
Mjumbe mwengine wa GIEI, Angela Buitrago, amesema baadhi ya maafisa wa umma ambao maagizo ya kukamtwa kwao yalitolewa miezi sita iliyopita, bado hawajakamatwa.
Hata hivyo, ofisi ya mwanasheria mkuu haikujibu ombi la kutoa tamko kuhusiana na kesi hiyo.