1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mexico yaikosoa Misri kwa mauaji ya raia wake

15 Septemba 2015

Mexico imeitaka Misri ichunguze kwa haraka kwa nini watalii waliuliwa kimakosa katika kile ambacho walioshuhudia wamekieleza kuwa ni shambulizi la kutokea angani lililosababisha vifo vya raia wawili wa Mexico.

https://p.dw.com/p/1GWZv
Mexiko Präsident Enrique Pena Nieto
Rais wa Mexico Enrique Pena NietoPicha: Reuters/E. Garrido

Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto alisema raia 14 wa Mexico walikuwa miongoni mwa watu waliohusika katika tukio la kusikitisha la Jumapili iliyopita katika jangwa la magharibi la Misri. Misri imesema maafisa wake wa usalama waliwaua kimakosa watu 12 na kuwajeruhi wengine 10 walipoushambulia msafara wao wakati walipokuwa wakiwafukuza wapiganaji wa jihadi. Hata hivyo hawajatoa taarifa kuhusu silaha zilizotumika wala maelezo kuhusu wahanga.

Rais Pena Nieto alituma risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa wahanga waliokufa katika hujuma hiyo iliyosababisha mshutuko nchini kote. "Mexico imetaka kutoka kwa serikali ya Misri uchunguzi wa kina na wa haraka kuhusu kilichotokea, utakaowawajibisha wahusika."

Misri imeahidi kuunda kamati maalumu kuchunguza kisa hicho itakayoongozwa na waziri mkuu Ibrahim Mahlab. Balozi wa Mexico nchini Misri, Jorge Alvarez Fuentes, amethibitisha Wamexico sita bado hawajulikani waliko huku mwanamke na mwanamume mmoja wakithibitishwa wamekufa. Waliojeruhiwa ni wanawake watano na mwanamume mmoja ambao wako katika hali nzuri.

Kairo Ägypten Touristen Unfall Terroristen Wüste
Magari yakipita jangwa la magharibi, MisriPicha: Reuters/Amr Abdallah Dalsh

Raia wa Mexico, Gabriela Bejarano amethibitisha kifo cha kaka yake Rafael Bejarano na kwamba mama yake amelazwa hospitalini. "Nimezungumza na rafiki yangu aliyeko huko na kitu pekee alichoniambia ni kwamba mama yangu yuko hospitalini na hali yake ni nzuri. Hayo tu ndiyo nijuayo, bado sijaongea naye." Gabriela alisema walikuwa jumla ya watalii 15, wengi wao wakitokea Guadalajara, na walitarajiwa kurejea Mexico Septemba 25.

Juhudi zafanywa kubaini kilichotokea

Akizungumza katika mji wa Mexico City balozi wa Misri nchini Mexico Yasser Shaban, ameviambia vyombo vya habari kuwa wizara za kigeni za mataifa hayo mawili zimekuwa zikiwasiliana kuthibitisha jinsi kisa hicho kilivyotokea. "Watalii wa Mexico walikuwa katika eneo la operesheni wakati wa harakati iliyofanywa na vikosi vya jeshi na polisi kuwalenga magaidi wanaotumia magari yanayofanana na yale yanayotumiwa na watalii, hali iliyosababisha watalii hao kushambuliwa kwa risasi na maafisa wa usalama."

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Mexico, Claudia Ruzi Massieu, amewaambia waandishi wa habari kuwa watalii sita wa Mexico walionusurika wamemfahamisha balozi wa Mexico nchini Misri kwamba walikuwa wamesimama mahali ili kupumzika na kula chakula wakati waliposhambuliwa kutokea angani kwa mabomu yaliyovurumishwa na ndege na helikopta. Kundi la watalii 14 wa Mexico liliwasili mjini Cairo Septemba 11 na kuondoka siku mbilii baadaye kuelekea eneo la Bahariya katika jangwa la magharibi.

Waziri Ruiz Massieu ameondoka Mexico jana jioni kuelekea Misri ambako anatarajiwa kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi ya juu kupata maelezo kuhusu kuuliwa kwa watalii wa Mexico ambao hawakuwa na hatia.

Mwandishi:Josephat Charo/afp/ape

Mhariri:Daniel Gakuba