1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi kutua Paris Saint Germain

10 Agosti 2021

Lionel Messi amewasili leo Jumanne kwenye uwanja wa ndege wa Barcelona kwa ajili ya kuabiri ndege hadi mjini Paris baada ya kuripotiwa kufikia makubaliano na klabu ya Paris Saint Germain.

https://p.dw.com/p/3ynwG
Frankreich Paris | Lionel Messi
Picha: Francois Mori/AP/picture alliance

Staa wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi amewasili leo Jumanne kwenye uwanja wa ndege wa Barcelona kwa ajili ya kuabiri ndege hadi mjini Paris baada ya kuripotiwa kufikia makubaliano na klabu ya Paris Saint Germain.

Gazeti la Ufaransa la L'Equipe limeripoti kuwa Messi, anatarajiwa katika mji mkuu wa Ufaransa Paris, kutia saini kandarasi na klabu hiyo inayotiwa makali na Mauricio Pochettino.

Messi, mwenye umri wa miaka 34 anashikilia rekodi ya ufungaji magoli katika timu yake ya taifa ya Argentina na klabu ya Barcelona, na anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji bora duniani katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Messi, mshindi wa tuzo ya mchezaji bora ya Ballon dor' mara sita, alitokwa na machozi mnamo siku ya Jumapili wakati alipokuwa akiiaga klabu yake ya tangu utotoni ya Barcelona baada ya klabu hiyo kusema haingeweza kumuhifadhi kutokana na sheria mpya za fedha za La Liga.

Wachambuzi wa soka wanasema kuwa safu ya ushambuliaji wa PSG ni ya kutisha kwani itakuwa na wachezaji nyota Neymar, Kylian Mbappe na sasa Messi.

Ujio wa Messi, utaiongezea nafasi klabu ya Paris Saint Germain ya kufanya vizuri katika mashindano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao.