1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Tutaharakisha hatua za kuwarejesha waliokosa hifadhi

17 Agosti 2018

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema serikali yake itaharakisha juhudi za kuwarudisha makwao wakimbizi wote ambao maombi yao ya kupewa hifadhi yamekataliwa.

https://p.dw.com/p/33Iqu
Deutschland Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/M. Skolimowska

Kauli hiyo ameitoa jana mjini Dresden baada ya mamia ya waandamanaji wanaofuata siasa kali za mrengo wa kulia kumtaka ajiuzulu kutokana na sera yake ya uhamiaji. Merkel alifanya ziara hiyo baada ya kumaliza mapumziko yake ya majira ya joto.

Eneo hilo la mashariki mwa Ujerumani ni ngome kuu ya wafuasi wengi wa chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia na kinachopinga wahamiaji, Chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD.

Merkel atetea uamuzi wake

Akizungumza katika mkutano wa faragha na wabunge wa chama chake cha Christian Democratic, CDU kwenye jimbo la Saxony, Merkel alirudia kuutetea uamuzi wake wa kuwakubali maelfu ya wahamiaji kwa kuzingatia ubinaadamu, lakini sasa ameahidi kuzuia kujirudia kwa hali kama hiyo na kusema kuwa atapambana na msingi wa kinachosababisha wahamiaji kukimbilia Ulaya.

''Kutokana na uhamiaji, nimeshasema wazi kwamba hali iliyoko sasa haimaanishi kwamba matatizo yote yametatuliwa. Hatua ya kuwarejesha wahamiaji makwao bado ni tatizo kubwa. Serikali ya shirikisho itachukua jukumu la kuwa makini zaidi hasa katika kupata nyaraka muhimu zinazohitajika, kama vile pasi za kusafiria. Lakini pia tutahakikisha kile kilichotokea mwaka 2015 hakitojirudia tena,'' alisema Merkel.

Deutschland Dresden Anti-Merkel Demonstration
Wafuasi walioandamana Dresden kumpinga MerkelPicha: DW/J. Chase

Merkal amesema anafahamu kwamba uamuzi wake kuhusu wakimbizi umewadhoofisha wapiga kura na kuzusha wasiwasi kuhusu uwezo wa serikali kulidhibiti suala hilo. Moja ya masomo ambayo Merkel amejifunza kutoka katika chama chake cha kihafidhina kwenye uchaguzi wa mwaka uliopita, ni kwamba alihitaji kufanya kazi nzuri zaidi ya kuwasiliana na watu wa kawaida kuhusu sera zake, hasa ile ya wahamiaji.

Mji wa Dresden umekuwa ukichukuliwa kama eneo adui kwa Kansela Merkel tangu Oktoba 3, mwaka 2016 wakati umati wa wafuasi wenye hasira na walio na msimamo mkali wa kulia waliposhangilia mitaani wakati wa sikukuu ya kuungana kwa Ujerumani kwa kuimba nyimbo za kumpinga Merkel.

PEGIDA na maandamano

Vuguvugu linalopinga Uislamu nchini Ujerumani la PEGIDA, liliandaa maandamano kuupinga uamuzi wa Merkel wa mwaka 2015 wa kuacha milango wazi kwa wakimbizi milioni moja, wengi wao wakiwa kutoka kwenye nchi za Kiislamu. Aidha, jana kiasi ya wafuasi 600 hadi 800 wa AfD na PEGIDA walikusanyika nje ya bunge la Saxony wakimtaka Merkel aondoke madarakani, huku wakionesha nia yao ya kutomkaribisha kwenye jimbo hilo na kumuita ''adui wa watu''.

Jimbo la Saxony linatarajiwa kupiga kura kuwachagua wabunge wa jimbo hilo Septemba mwaka ujao wa 2019 na utafiti wa maoni unaonesha kuwa chama cha AfD huenda kikaibuka cha pili chenye nguvu, huku CDU bila shaka kikishika nafasi ya kwanza.

Katika uchaguzi wa mwaka uliopita, chama cha AfD kilishinda na kuwa chama kikuu cha tatu katika bunge la Ujerumani, hatua iliyozifanya juhudi za Kansela Merkel kuunda serikali mpya ya muungano kuwa ngumu zaidi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, DW https://bit.ly/2wauJ3E
Mhariri: Josephat Charo