Merkel na viongozi wa Ulaya waahidi kusimama pamoja
29 Juni 2017Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema kwamba watashirikiana kutia msukumo kuhusu mtizamo wao juu ya mabadiliko ya tabia nchi pamoja na biashara huru katika mkutano wa kundi la nchi tajiri kiviwanda na zile zinazoinukia kiuchumi wa G20 wiki ijayo. Hata hivyo viongozi hao pia wameweka wazi kwamba watajaribu kumtenga rais wa Marekani Donald Trump ambaye amekwisha kujiweka pembeni na kukataa kushirikiana na viongozi wenzake. Kansela Merkel ambaye amekutana na viongozi wengine mjini Berlin hii leo amesema nchi za Ulaya zinataka kutuma ujumbe wa kujitolea katika mkutano wa kilele utakaofanyika mjini Hamburg Julai 7 hadi 8.
Katika mkutano uliofanbyika leo hii mjini Berlin ulioongozwa na Kansela Merkel,rais wa Ufaransa Emanuel Macron alionesha kuwa na matarajiio kwamba Marekani itafikiria tena msimamo wake na kurudi kwenye mstari wa kuelewa mambo baada ya kutangaza kwamba itajiondoa kwenye mkataba wa tabia nchini ulioafikiwa mjini Paris Ufaransa.Lakini pia rais huyo wa Ufaransa ameongeza kusema kwamba ni jambo lisiloingia akili hata mara moja kumtenga Trump akisema Ulaya ina ushirika mkubwa mno na Marekani ikiwemo kuwa na mtizamo sawa kuhusu ugaidi kama tatizo linalohitajika kukabiliwa kwa pamoja.
''Tunafungamanishwa na mengi na Marekani. Tunashirikiana katika mapambano dhidi ya ugaidi,kanuni za kimataifa na masuala mengi yawe ni kuhusu Afrika au katika Mashariki ya Kati. Tunafanya kazi na Marekani. Tunawahitaji katika kiwango cha kijeshi kama ilivyo katika kiwango cha ushirikiano wa kiusalama.''
Kansela Merkel kwa upande wake akizungumza katika mkutano huo aliyouongoza mjini Berlin amesema Ulaya itashirikiana kuelekea mkutano wa kilele wa G20 kwa ajili ya kuüpata suluhisho la pamoja na Marekani katika suala hilo hilo la mabadiliko ya tabia nchi na masuala mengine.Kwa waandishi wa habari Merkel amebaini kwamba Marekani ni sehemu muhimu ya kundi la G20 na kwamba pamoja na washiriki wa Umoja wa Ulaya kusimama pamoja kuelekea mkataba wa Paris hata baada ya utawala wa Trump kuamua kujiondoa kwenye mkataba huo kama Ulaya watafanya kazi pamoja kutafuta suluhu ya suala hilo na masuala mengine katika mkutano wa Hamburg.
''Kwasababu ya Marekani kujiondia katika mkataba wa Paris kuhusu tabia nchi bila shaka kuna maeneo ambako tunatafautiana.Lakini Marekani ni sehemu kubwa ya G20 na hiyo ndiyo sababu tutafanya kila tuwezalo kushirikiana nao na bila ya kuzigusia tafauti zetu''
Mkutano huu wa leo mjini Berlin Merkel alikuwa pamoja na viongozi wenzake wa Ufaransa, Italia, Uholanzi, Uhispania na Norway pamoja na wajumbe wa Umoja wa Ulaya. Kiongozi huyo wa Ujerumani leo hii pia amewaambia wabunge wa Ujerumani kwamba Umoja wa Ulaya umejitolea kushinda ilivyokuwa huko nyuma kuhakikisha mkataba wa Paris dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi unafanikiwa. Amewahutubia wabunge mjini Berlin na kuwahakikishia kwamba mkataba huo wa Paris hauwezi kubadilishwa na hauwezi kuwekwa pembeni wala hakuna mjadala kuhusu hilo.
Wakati huo huo, Ujerumani imetowa taaarifa ya kulikataa ombi la rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan la kutaka kupata fursa ya kuwahutubia waturuki wanaoishi Ujerumani wiki ijayo pale atakapokuwa amekuja kuhudhuria mkutano wa G20. Hata hivyo jibu la Ujerumani limewakasirisha viongozi wa mjini Ankara katika wakati ambapo uhusiano baina ya serikali hizo mbili unazidi kuporomoka kutokana na hatua ya Uturuki kuwaandama wapinzani kufuatia mapinduzi yaliyoshindwa dhidi ya serikali ya Erdogan.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema amepokea ombi hilo la rais Erdogan la kutaka fursa ya kuwahutubia waturuki karibu milioni 3 wanaoishi nchini Ujerumani pembezoni mwa mkutano wa G20.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Khelef