1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na mawaziri wake wazungumzia ustawi

11 Aprili 2018

Baraza la mawaziri la Ujerumani limekubaliana kuwa uchumi ulio imara na nafasi za ajira ndio masuala ya kupewa kipaumbele, baada ya kushuhudia wiki za mwanzo zenye changamoto kwa serikali mpya ya Kansela Angela Merkel

https://p.dw.com/p/2vpwR
Deutschland Klausurtagung des Bundeskabinetts
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Waziri wa uchumi Peter Altmaier alisema kwenye mkutano huo kuwa mawaziri wataangazia katika kuuweka uchumi wa Ujerumani katika hali nzuri na kujitahidi kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ustawi. "Tuna jukumu la kutetea maslahi ya Ujerumani katika midahalo ya kimataifa kuhusu sera za biashara na masoko ya wazi. Lazima tuhakikishe tunajiandaa vilivyo. Tumejadili haya yote na mashirika makuu ya uchumi wa Ujerumani, pamoja na waajiri na waajiriwa"

Merkel aliingia madarakani kwa muhula wake wa nne mwezi uliopita baada ya kuongoza mazungumzo marefu ya kuunda muungano kati ya chama chake cha Christian Democratic Union – CDU, washirika wake Christian Social Union – CSU na chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic Union – SPD.

PK Ergebnisse der Steuerschätzung
Waziri wa Uchumi Peter Altmeier asema uchumi uko imaraPicha: picture alliance/dpa/W. Kumm

Mawaziri wa Merkel walianza kuweka mpango wa utendaji kazi wa serikali kwa ajili ya miezi 12 ijayo katika mkutano wa siku mbili ulioanza jana kwenye kasri la Meseberg, nje ya mji mkuu Berlin. Mkutano huo utakamilika leo.

Miongoni mwa mada ambazo yeye na mawaziri wake 15 wa serikali wanatarajiwa kujadili ni bajeti ijayo, itakayotayarishwa na Waziri wa Fedha wa chama cha SPD Olaf Scholz.

Serikali hiyo ya muungano inataka kupunguza idadi ya wasio na ajira, ikiwa ni pamoja na kujaribu kuwaingiza katika nguvu kazi karibu watu 150,000 wasio na ajira za kudumu kwa kutengeneza kazi ambazo waajiri wanapewa ruzuku na serikali ya kiasi cha karibu euro bilioni moja kwa mwaka.

Wakati mawaziri wakionekana kuzungumza kwa sauti moja katika mkutano huo, wiki chache zilizopita zilikumbwa na hali ya kutoelewana

Mwishoni mwa wiki, kiongozi wa kundi la wabunge la SPD, Andrea Nahles, alimkosoa kiongozi wa chama cha CSU Horst Seehofer kwa matamshi yenye utata ambayo yaligonga vichwa vya habari wiki chache zilizopita.

Deutschland Klausurtagung der Bundesregierung auf Schloß Meseberg | Jens Stoltenberg
Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg pia anahudhuriaPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Nahles alisema kuwa mwanasiasa huyo anayepinga vikali sera za uhamiaji, ambaye msimamo wake ulimuweka katika mgongano na Merkel anataka tu kuiimarisha sifa yake, badala ya kuitumikia nchi. Seehorfer alijibu Jumatatu akisema Wasocial Democrats wanapaswa kuwa watulivu.

Nahles ameamua kubakia nje ya baraza la mawaziri, na badala yake kuliongoza kundi la wabunge wa SPD – jukumu ambalo linalomuwezesha kuishinikiza serikali kupitisha mageuzi muhimu kwa wanachama wa chama chake na kuwakosoa wahafidhina wa Merkel.

Shinikizo liko kwenye pande zote mbili kutimiza ahadi zao. Makubaliano ya muungano huo yanajumuisha kipengele kinachotoa nafasi ya kutathmini hatua zilizopigwa na serikali baada ya miaka miwili – na kuupa kila upande fursa ya kuondoka kwenye muungano huo kama hali haitakuwa nzuri kwao.

Rais wa Halmashauri Kuu ya UIaya, Jean-Claude Junker, na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihamin ya NATO, Jens Stoltenberg, pia wanahudhuria mazungumzo hayo ya baraza la mawaziri wa Merkel.

Wanatarajiwa kujadili jukumu la Umoja wa Ulaya katika ulimwengu, kuimarisha usalama katika mipaka ya Umoja wan Ulaya na kuimarisha ushirikiano na bara la Afrika.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef