Merkel azuru India
1 Novemba 2019Hali ya hatari kwa afya imetangazwa mjini New-Delhi na katika maeneo ya karibu na hapo hii leo baada ya eneo hilo kufunikwa na hewa chafu ya hali ya juu. Mamlaka inaaoshughulikia udhibiti wa hewa chafu imepiga marufuku pia harakati zote za viwanda na ujenzi hadi Novemba tano inayokuja. Barakoa milioni tano zimesambazwa kwa wanafunzi na familia zao. Hali hii inajiri wakati kansela wa ujerumani Angela Merkel na ujumbe wake wamewasili mjini New-Delhi tangu jana alkhamisi kwa ziara rasmi ya siku mbili.
Katika sherehe za kumkaribisha katika kasri la waziri mkuu asubuhi kansela Merkel hakuvaa chombo chochote cha kumkinga dhidi ya hewa chafu licha ya kiwango cha juu cha hewa chafu.
Viongozi wote wawili kansela Merkel na mwenyeji wake waziri mkuu Narendra Modi hawakufuata ushauri wa wahudumu wa afya walipokagua vikosi vya wanajeshi. Lakini wakati wimbo wa taifa ulipokuwa unapigwa kansela Merkel aliketi kidogo ili kuepukana na kisa kama kile cha kutetemeka kilichowahi kutokea mapema mwaka huu.
Kansela Merkel amemshukuru waziri mkuu Modi kwa mapokezi ya dhati .
Serikali ya Ujerumani na ile ya India wanadhamiria kuimarisha ushirikiano wao katika masuala yatakayoishughulisha zaidi dunia siku zinazokuja mfano akili ya kubuni, digitali na pia mabadiliko ya tabianchi. "India ina uwezo mkubwa katika fani hizo" amesema kansela Merkel huku waziri mkuu wa India Narendra modi akizungumzia ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.
Kansela Merkel na mwenyeji wake Narendra Modi wamekubaliana pia kuimarisha juhudi za kuanzishwa upya majadiliano kuhusu makubaliano ya biashara huru kati ya Umoja wa ulaya na India mazungumzo yaliyokwama tangu mwaka 2013.
Wawakilishi wa serikali za nchi hizi mbili wametiliana saini mikataba zaidi ya 20 ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo kuepusha balaa la takataka baharini, usafiri unaoheshimu usafi wa mazingira katika miji, matibabu ya jadi ya ayuverda hadi kufikia yoga.