Merkel atetea uamuzi wa benki ya Ulaya, ECB
8 Septemba 2012Rais wa benki kuu ya Ulaya, ECB Mario Draghi amewasilisha mipango siku ya Alhamis ya kununua dhamana kwa kiasi kisicho na ukomo zinazopevuka katika muda wa miaka mitatu zilizotolewa na mataifa ambayo yameomba fedha za uokozi kutoka mfuko wa uokozi wa Ulaya na kutimiza masharti magumu ya sera za ndani. Mkuu wa benki kuu ya Ujerumani alikuwa pekee aliyepinga mpango huo wakati wa kufikiwa uamuzi huo.
Vyama vinavyounda serikali ya mseto vya nadharia za mrengo wa kati-kulia vinaendelea kwa kiasi kikubwa kuwa nyuma ya msimamo wa Merkel wa kuunga mkono wa kuyapa msaada mataifa yaliyo katika matatizo kama Uhispania na Italia lakini kwa masharti kuwa yanatekeleza mageuzi magumu ya kifedha katika nchi zao.
Kuna malalamiko
Lakini malalamiko kutoka kwa kundi dogo lakini lenye sauti linalotia shaka shaka kuhusu mradi wa Ulaya miongoni mwa wabunge wa chama cha Kansela Merkel pamoja na vyombo muhimu vya habari vya kihafidhina yanaonyesha hofu ya kisiasa katika kipindi kinachoelekea kwenye uchaguzi ambao utafanyika mwaka mmoja kutoka hivi sasa.
ECB ni taasisi huru na yenye nguvu kubwa , Merkel amewaambia waandishi habari mjini Vienna, akisisitiza kuwa msaada utatolewa ukiambatana na masharti, hayo yakiwa ni matamshi yake ya kwanza kuhusiana na mpango huo.
''Masharti ni suala muhimu sana. Udhibiti na msaada, ama udhibiti na masharti, vinakwenda sambamba''. amesema Merkel.
Wajerumani wana wasi wasi
Lakini Wajerumani wengi wahafidhina wanakubaliana na wasi wasi wa Jens Weidmann , mkuu wa benki ya Ujerumani, Bundesbank, kuwa mpango wa ununuzi wa dhamana unakwenda kinyume na suala nyeti la kuyapa fedha mataifa yenye nakisi katika bajeti zao, kuondoa mbinyo kutoka katika serikali wa kufanya mageuzi na hatimaye utaongeza ughali wa maisha.
Kuyapatia fedha za bure mataifa yenye madeni, ilikuwa kichwa cha habari katika gazeti lenye wasomaji wengi la Bild, ikiwa ni ukosoaji mkali kwa mikopo iliyopatiwa Ugiriki pamoja na mataifa mengine ya eneo la euro ambayo yamo katika matatizo, na kuongeza kuwa hatua ya ECB inaweza kuiporomosha sarafu ya euro.
Uchunguzi wa maoni
Uchunguzi wa maoni uliotolewa Alhamis, (06.09.2012) kabla ya mpango wa ununuzi wa dhamana kutangazwa unaonesha karibu Mjerumani mmoja kati ya wawili hawana imani na Draghi, ambaye ni Mtaliani.
Wabunge kadha wameapa kuchukua hatua ya kisheria kuzuwia mpango huo. ''Tunapaswa kufikiria kuchukua hatua za kisheria kuangalia iwapo ECB imekiuka kwa kiasi kikubwa mamlaka yake. Nina hakika kuwa hii ndio hali halisi''. Amesema Klaus-Peter Willsch, mbunge ambaye hana imani na mradi wa Ulaya moja kutoka chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union, CDU, katika mazungumzo na radio ya Ujerumani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba.