1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akabiliwa na pigo jengine la uchaguzi jimboni Hesse

27 Oktoba 2018

Jimbo la Hesse lililopo katikati ya Ujerumani litapiga kura muhimu kwa mustakabal wa Kansela Angela Merkel Jumapili hii, wiki mbili tu baada ya uchaguzi wa jimbo la Bavaria ambako wahafidhina walipata pigo kubwa.

https://p.dw.com/p/37Gc1
Deutschland, Fulda: Der hessische Ministerpräsident Volker Bouffier Bundeskanzlerin Angela Merkel nehmen an der letzten Wahlkampagne vor den bevorstehenden Landtagswahlen teil
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa jimbo la Hesse Volker Bouffier wakiwa katika kampeni za mwisho kabla ya uchaguzi wa Jumapili.Picha: REUTERS

Kwa mara nyingine mnamo muda wa wiki mbili serikali ya mseto ya Ujerumani inajiandaa kuchapwa tena katika uchaguzi wa hapo Jumapili kwenye jimbo la kati la Hesse.

Mji wa Frankfurt ambao ni makao makuu ya shughuli za fedha  uko katika jimbo hilo ambalo kwa kipindi cha miaka 20 limekuwa ngome kuu ya wahafidhina.

Hata hivyo wachambuzi wanasema kimsingi hakuna haja ya kuwa na kiherehere, sababu ni kwamba jimbo hilo lina idadi ndogo kabisa ya watu wasiokuwa na ajira na uchumi wake unastawi vizuri sana. Lakini  uchaguzi huo siyo wa kawaida katika jimbo hilo.

Kulingana na uchunguzi wa maoni chama cha Kansela Merkel cha CDU kinatarajiwa kupata asilimia 28 ya kura katika uchaguzi wa kesho, yaani pungufu ya asilimia 12 kulinganisha na uchaguzi wa  mwaka 2013.

Katika uchaguzi wa jimbo la Bavaria wiki mbili zilizopita ni washirika wa kansela Merkel wa Christian Social  Union waliopata pigo kubwa. Lakini katika uchaguzi wa jimbo la Hesse ni chama chake cha CDU kinachotarajiwa kupata pigo. Ikiwa  kitashindwa vibaya serikali ya mseto inayoongozwa na kansela Merkel inaweza kusambaratika.

Infografik Sonntagsfrage Hessen EN
Matokeo ya uchunguzi wa maoni kuhusu uchaguzi wa jimbo la Hesse.

Waziri mkuu wa jimbo la Hesse Volker Bouffier ameiambia DW kwamba anayo matumaini ya kushinda vizuri  katika uhaguzi wa kesho. Lakini ni kweli kwamba yanayotokea kwenye serikali kuu yanaathiri siasa za  majimboni.

Vyama vikuu vya CDU na SPD vinapewa changamoto kubwa na vyama vidogo vya kijani na kile cha mrengo mkali wa kulia AFD.

Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa chama cha Kijani kitafikia asilimia kati ya 20 na 22 na AfD asilimia 13, kwa mara ya kwanza chama hicho kinatarjiwa kuingia katika bunge la jimbo la Hesse na hivyo kuwakilishwa katika mabunge ya majimbo yote ya Ujerumani.

Chama cha Angela Merkel CDU kitakuwamo mashakani ikiwa chama cha kijani kitapata kura zaidi. Na ikiwa chama kingine kikuu SPD nacho kitaboronga katika uchaguzi wa kesho miito ya kukitaka chama hicho kijiondoe kwenye serikali ya mseto itazidi kuwa ya sauti za juu.

Ikiwa chama cha SPD kitachuka hatua ya kujiondoa kwenye serikali ya mseto, serikali hiyo itadhoofika na katika upande mwingine imani juu ya Kansela Merkel kuweza kuidumisha serikali hiyo itatiliwa mashaka. Hali hiyo itazusha maswali juu ya mustakabal wa serikali kuu ya Ujerumani.

Mwandishi: Zainab Aziz/p.dw.com/p/37DXQ

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman