Merkel ahimiza ushirika wa dunia katika maendeleo
26 Septemba 2015Viongozi wa dunia Ijumaa (25.09.2015) wamepitisha mpango wa malengo ya maendeleo kutokomeza umaskini uliokithiri duniani ifikapo mwaka 2030.
Malengo ya Maendeleo Endelevu yanakusudia kutokomeza umaskini uliokithiri, kupambana na ukosefu wa usawa na dhuluma,kutowa elimu bora kwa watu wote na kufanikisha ukuaji wa kiuchumi ifikapo mwaka 2030.
Viongozi wa dunia waliidhinisha agenda hiyo kuu katika mkutano wa kilele wa ngazi ya juu muda mfupi kabla ya ya mkutano huo wa wiki moja wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuadhimisha miaka sabini ya chombo hicho cha dunia.Agenda ya mpango huo wa malengo endelevu ni matokeo ya mazungumzo yaliokuwa yakifanyika kwa miaka mingi na serikali na mashirika ya kiraia.
Akihutubia Baraza hilo Kuu la Umoja wa Mataifa Kansela Angela Merkel ametowa wito wa kuwepo ushirika wa dunia kufanikisha malengo hayo ya maendeleo na ameahidi kuongeza bajeti ya Ujerumani kwa ajili ya suala la maendeleo.
Merkel amekaririwa akisema " Kila mmoja wao anapaswa kufanya kazi na lazima afanye kazi ya kutekeleza agenda hiyo.
Fedha zaidi kwa malengo ya maendeleo
Ujerumani itatimiza wajibu wake wa kutenga asilimia 0.7 wa pato lale la jumla la ndani ya nchi kugharamia maendeleo na pia itaongeza mchango mkubwa katika suala la maendeleo.
Merkel amesema ni muhimu kwa nchi zenye maendeleo ya viwanda duniani kutimiza ahadi zao na kwamba Ujerumani itatowa mchango wake kufanikisha jambo hilo kwa kutowa dola bilioni 100 kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kuhifadhi mazingira kuanzia mwaka 2020 jambo ambalo amesema litazidisha imani na kuwafanya watu waishi maisha yenye heshima.
Wakati akipongeza malengo hayo mapya ya maendeleo amesisitiza kwamba amani ni sharti muhimu la kufanikisha maendeleo.
Mzozo wa wahamiaji lazima ushughulikiwe
Akizungumzia mzozo wa wahamiaji barani Ulaya kiongozi huyo wa Ujerumani amesema kila mtu anayeshuhudia kuteseka kwa wale wanaokimbia nchi zao kutafuta hifadhi na wale wanaojuwa changamoto inazokabili nchi inazowapokea wakimbizi hao anaweza kutambuwa kwamba mwishowe kuna suluhisho moja kwamba lazima washughulikie sababu ya mzozo huo wa wahamiaji.
Merkel amesema mamilioni ya wakimbizi na wahamiaji wanaukimbia "ugaidi na matumizi ya nguvu ".Ujerumani inatarajia kupokea maombi ya kutaka hifadhi 800,000 mwaka 2015 na kwa mujibu wa takwimu nyengine idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia hata milioni moja.
Serikali ya Ujerumani na zile za majimbo zimekubaliana juu ya mpango wa hatua za kukabiliana na wimbi hilo kubwa la wahamiaji wanaokimbilia nchini.Fedha zaidi zitatumwa kwa kila jimbo kwa kutegemea idadi ya wakimbizi inaowapokea.Kila jimbo litapokea euro 670 atakazopewa kila mhamiaji kwa mwezi.
Mara tu baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kilele viongozi wa dunia wataanza mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo Jumatatu ambapo suala la vita vya Syria na mzozo wa wahamiaji yanatazamiwa kuhodhi agenda.
Kansela Merkel ni miongoni mwa viongozi tisa kutoka kanda tafauti ambao watafanya kazi kuhakikisha utekelezaji wa malengo hayo ya maendeleo. Wengine ni marais wa Brazil, Clombia,Liberia,Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia na mawaziri wakuu wa Sweden na Timor Mashariki.
Jumamosi Kansela Merkel anatembelea eneo la "Ground Zero " ambacho ni kitovu cha shambulio la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001 katika mji wa New York nchini Marekani.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP//AFP/dpa
Mhariri : Yusra Buwayhid