Merkel aahidi msaada kwa waliokumbwa na mafuriko
18 Julai 2021Akizungumza siku ya Jumapili baada ya kuwasili kwenye mji wa Schuld, moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko, Merkel ameielezea hali katika maeneo hayo kuwa ya kutisha.
Merkel ambaye ameahidi msaada wa haraka wa kifedha pia amezipongeza juhudi za uokozi zinazoendelea na mshikamano aliouona wakati wa ziara hiyo, lakini ameonya kwamba shida kwenye eneo hilo hazitotatuliwa haraka.
"Nimekuja kushuhudia picha halisi isiyo ya kawaida. Tutasimama Pamoja katika hili kwa kuwa na suluhisho la muda mfupi, lakini pia la kati na la kudumu," alisisitiza Merkel.
Misaada kuanza Jumatano
Kansela huyo wa Ujerumani amesema msaada wa muda mfupi utazinduliwa na serikali siku ya Jumatano.
Merkel amesema Ujerumani inahitaji sera ambayo inazingatia mabadiliko ya tabianchi kuliko ilivyofanyika katika miaka ya hivi karibuni. Kiongozi huyo ameahidi kufanya juhudi zaidi kujilinda na athari zitonakazo na mabadiliko ya tabianchi.
Merkel ameutembelea pia mji wa Ahrweiler kwa mara ya kwanza tangu aliporejea kutoka nchini Marekani kwenye ziara yake ya mwisho kabla ya kuondoka madarakani baada ya uchaguzi wa mwezi Septemba.
Merkel alikuwa ameongozana na Malu Dreyer, Waziri Mkuu wa jimbo la Rhineland-Palatinate. Maafa hayo yamesababisha vifo vya watu 110 katika wilaya ya Ahrweiler iliyoko kwenye jimbo hilo na watu wengine 670 wamejeruhiwa. Vifo vingine 46 vimeripotiwa katika jimbo jirani la North-Rhine Westphalia.
Dreyer amesema ni jambo jema kwamba Merkel amewatembelea, kwani wasingeza kulitatua tatizo hilo peke yao. Amesema utayari wa watu wa eneo hilo kusaidia ni mkubwa sana.
Takriban watu 60 bado hawajulikani walipo katika mji wa Erftstadt magharibi mwa Cologne. Wakaazi kadhaa bado wanasubiri kupata taarifa kuhusu wapendwa wao.
Mbali na Ujerumani, mafuriko hayo pia yamezikumba nchi za Ubelgiji, Uholanzi na Austria. Ubelgiji imethibitisha vifo vya wati 27.
Nalo eneo la kusini mashariki mwa Ujerumani pia limekumbwa na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa. Msemaji wa wilaya ya Bavaria amesema mtu mmoja amekufa katika mji wa Berchtesgadener Land.
Jimbo la Bavaria limewaondoa watu 130 kutoka kwenye makaazi yao yaliyoko Berchtesgadener Land karibu na mpaka wa Austria. Maafisa waliwaambia watu kutoka Schönau am Königssee kuondoka kwenye nyumba zao.
Papa awaombea waliokumbwa na mafuriko Ulaya
Naye kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameyataja mafuriko yaliyosababisha vifo nchini Ujerumani, Ubelgiji na Uholanzi kuwa maafa. Akizungumza katika hotuba zake za kila wiki, kwenye uwanja wa Mtakatifu Peter, Papa Francis amesema anawaombea watu wote wa Ulaya waliokumbwa na mafuriko.
Papa mwenye umri wa miaka 84, amemuomba Mwenyezi Mungu azipokee roho za watu waliokufa kutokana na mafuriko hayo pamoja na kuzifariji familia zao.
Aidha, timu ya Ujerumani inayoshiriki michezo ya Olimpiki mjini Tokyo yenye wanariadha 80, ilikaa kimya kwa dakika moja siku ya Jumapili kuwakumbuka watu waliokufa katika mafuriko hayo. Shirikisho la Michezo ya Olimpiki la Ujerumani, DOSB tayari limetenga Euro 100,000 kama msaada wa dharura.
Kwa upande wake Rais mpya wa Israel, Issac Herzog amemuandikia barua Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier kutoa pole kwa watu wa Ujerumani kutokana na vifo na uharibifu mkubwa uliosababishwa na mafuriko. Wasaidizi wa Rais Herzog wamemwambia Steinmeier kwamba Israel ni mshirika katika juhudi au mipango yoyote ile yenye lengo la kushughulikia haraka changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
(DPA, AP, AFP, Reuters)