1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahalo wa vyama vidogo watikisa Ujerumani

5 Septemba 2017

Macho yatakodolewa kuona mshindi wa tatu baada ya uchaguzi wa tarehe 24 Septemba,mshindi huyo huenda akawa muamuzi wa serikali itakayoshika usukani

https://p.dw.com/p/2jMpe
Deutschland - Live-Fünfkampf der kleinen Parteien in der ARD
Picha: picture-alliance/B. v. Jutrczenka

Wagombea walioko katika nafasi ya juu wa  vyama vidogo nchini Ujerumani wamekabiliana katika mjadala kuhusu masuala muhimu yanayolihusu taifa kwa ujumla na zaidi juu ya masuala ya uhamiaji,usalama na mambo ya nje.Mdahalo huo wa Televisheni umefanyika jana Jumatatu. Ni tukio ambalo limekuja ikiwa zimebakia chini ya wiki tatu kabla ya wajerumani kuteremka vituoni kupiga kura katika uchaguzi mkuu ambapo kila mmoja anasubiri kuona ni chama gani katika vyama hivyo vidogo kitaibuka kuchukua nafasi ya tatu ambayo huenda ndicho kitakachokuwa chama kitakachoamua muundo wa serikali mpya itakayoingia madarakani.

Mapambano katika mdahalo wa Televisheni kati vyama vodogo vya Ujerumani yamefuatia mdahalo kama huo kati ya wagombea wakuu wawili Kansela Angela Merkel ambaye ni mwanasiasa wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Christian Democratic Union CDU na upande mwingine mpinzani wake kutoka chama cha Social Democtic SPD Marztin Schultz mnamo siku ya Jumapili ambapo wengi wanahisi hakuna tafauti kubwa iliyojitokeza baina yao. Hali hiyo imeibua atiati kwamba dalili zote zinaonesha uwezekano mkubwa wa kurudi tena kwa serikali ya mseto wa vyama hivyo viwili vikuu yaani CDU na chama ndugu CSU pamoja na SPD baada ya uchaguzi wa tarehe 24.

Infografik Sonntagsfrage Bundestagswahl 25.08.2017 ENG

Hata hivyo wagombea wote wawili Merkel na Schultz wameshasisitiza kwamba wanataka kuepusha hali hiyo isitokee.Lakini kura za maoni tayari zinaonesha kwamba  serikali mpya itakuwa na wingi madhubuti pale tu itakapopatikana serikali ya mseto wa vyama vikuu au ikiwa itaundwa serikali ya mseto wa vyama vitatu kati ya wahafidhina yaani CDU/CSU,chama cha kijani na chama kinachopendelea zaidi masuala ya kibiashara cha Free Demokratic FDP.Katika mdahalo wa vyama vidogo uliofanyika jana Jumatatu Cem Özdemir kutoka chama cha kijani au wanamazingira alimshambulia sana mgombea wa chama cha Kushoto Die Linke Sahra Wagenknecht na mwanasiasa wa AFD Alice Weidel kwa misimamo yao juu ya kutoupendelea umoja wa Ulaya.

''Sipendi hizi kauli ambazo zinapinga umaarufu wa Umoja wa Ulaya iwe ni kutoka mrengo wa Kushoto au Kulia.Nahisi hizi kauli  ni za kutafuta sababu za kushindwa kwa siasa za kitaifa kwa kuibebesha lawama benki kuu ya Umoja wa Ulaya,kanda ya Yuro au Brussels.Siwezi kuvumilia hata kidogo kauli hizi.Ujerumani inapata faida kutoka Umoja wa Ulaya kuliko nchi nyingine nyingi. Hata katika mgogoro kuhusu Ugiriki tulipata faida kutokana na mgogoro huo na huo ndio ukweli.Ujerumani inapata manufaa kutoka Umoja wa Ulaya.''

Weidel kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachopinga wageni cha AFD ameilaumu sana benki kuu ya Umoja wa Ulaya kwa sera zake za usimamizi wa fedha ambazo anasema zimechangia kuongezeka kwa gharama za kukodi nyumba na bei za majumba katika miji ya Ujerumani na kuishutumu benki hiyo kwamba imekiuka mikataba ya Umoja wa Ulaya katika mpango wake wa kununua zabuni. Lakini kwa upande mwingine mgombea wa chama cha FDP Christian Lindner  akajaribu kumbana Özdemir kwa kumtuhumu kuwa ndumalakuwili linapokuja suala la sera za nje na kusema amekuwa mara nyingi akijiegemeza na Urusi.

Deutschland - Live-Fünfkampf der kleinen Parteien in der ARD: Christian Lindner
Picha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Nchi ambayo imekuwa ikikosolewa na kulaaniwa na hata kansela Merkel kwa kulinyakua kwa mabavu jimbo la Crimea pamoja na kuunga mkono waasi wanaoipinga serikali walioko mashariki ya Ukraine.Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Emnid siku ya Jumapili umeonesha kwamba chama cha SPD kimejiongezea pointi moja asilimia  na kukifanya kuwa na asilimia 24 wakati chama cha Merkel kikibakia katika asilimia 38,chama cha Die Linke  kina asilimia 9 na kuwa chama cha tatu chenye nguvu huku wanamazingira FDP na AFD wakishikilia asilimia 8 kila mmoja.

Hii inaamanisha kwamba vyama sita vinatarajiwa kuingia bungeni safari hii kutoka vyama vinne.

Mwandishi:Saumu Mwasimba RTRE/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW