Mdahalo wa kuingilia kijeshi Syria
14 Februari 2016Na kuna funzo moja kubwa lililojitokeza katika mijadala hiyo katika siku ya mwisho ya mkutano wa usalama mjini Munich Jumapili (14.02.2016) nalo ni : Kuingilia kati kijeshi kunaweza kuwa halali na ni zana inayofaa kubadili matukio nchini Syria na kuzuwiya au kupunguza maafa ya kibinaadamu.
Matumaini ya kufikiwa suluhu kwa amani na kufikishwa kwa haraka misaada ya kibinaadamu katika maeneo yaliyozingirwa nchini Syria leo yamedidimia wakati vikosi vya serikali vikisaidiwa na mashambulizi ya anga ya Urusi dhidi ya waasi vikisonga mbele kuelekea jimbo la kaskazini la Allepo.
Seneta John McCain wa Marekani,Riyad Hijab mjumbe mkuu wa upinzani wa Syria na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson ni miongoni mwa wanadiplomasia na wataalamu wa sera za kigeni kuelezea mashaka yao makubwa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kupeleka misaada kufikia wiki ijayo.
Kujititimuwa kwa Urusi
McCain Amesema mashaka yake hayo yanatokana na tabia ya hasimu yao Urusi ya kutaka kuwa na ushawishi mkubwa duniani na kwamba hatua ya Rais Putin kuingilia kati nchini Syria ni jaribio la kuirudisha Urusi kama taifa kubwa kwa kuuchochea mzozo wa wakimbizi ili kuigawa jumuiya ya kujihami ya NATO na kuyumbisha Umoja wa Ulaya.
Amesema busara haitomaliza mzozo huo wa Syria na kwamba makubaliano hayo yataiwezesha tu Urusi kijeshi.
Ametaka ifahamike wazi kwamba makunaliano hayo : "Yanaruhusu kuendelea kwa mashmabulizi dhidi ya Allepo kwa wiki nyengine.Inayataka makundi ya upinzani kusitisha mapigano lakini inaruhusu Urusi kuendelea kuwashambulia magaidi ambao inasisitiza kuwa kila mtu wakiwemo raia."
Kundi la nchi 17 la kuisaidia Syria likiwa chini ya uenyekiti wa Urusi na Marekani limekubalina hapo Ijumaa kutafuta usitishaji wa uhasama nchini Syria katika kipindi kisichozidi wiki moja na kundaa haraka mpango wa kufikisha misaada kwa maeneo yaliyozingirwa nchini humo.
Kuigilia kati kijeshi
Kwa waziri wa ulinzi wa Norway Ine Eriksen Soreide Syria ni mfano mkuu wa kuingiliwa kati kiijeshi.Amesema hatua za kijeshi zinahitajika kubadili hali ya mambo nchini Syria kwamba "Shauku ya kufikia suluhisho la kisiasa imekuwa ikipunguwa kila dakika kwa mtazamo wa Assad". akimaanisha rais wa Syria ambaye amepata nguvu kutokana na msaada wa mashambulizi ya anga yanayofanywa na Urusi nchini Syria.
Kauli yake imeungwa mkono na Anne- Marie Slaughter mkurugenzi wa zamani wa mipango ya sera katika Wizara ya mambo ya nje ya Marekani chini ya uongozi wa Rais Barack Obama na hivi sasa ni mkuu wa Wakfu Mpya wa Marekani mjini Washington.
Mkuu wa ujumbe wa upinzani Riyad Hijab ameishutumu Urusi na serikali ya Syria kwa kuwa na mkakati wa kuwapotezea watu makaazi kwa nguvu na kwamba hakuna kati yao mwenye utashi na suluhu.
Kusita kuingilia kijeshi
Mhariri wa gazeti la Financial Times Roula Khalef ametowa ufafanuzi madhubuti kwa kile kinachoonekana kuwa kusita kwa mataifa mengi kutimiza dhima madhubuti zaidi katika mzozo wa miaka mitano wa Syria.
Amesema "Tumejifunza kutoka Vita vya Iraq.Vita hivyo vilianzishwa kwa visingizio vya uwongo na haukuwa uingiliaji kati kwa misingi ya kibinaadamu na umeishia kwa maafa ambayo yanatuandama hadi leo hii.
Uingiliaji kati wa hivi karibuni kabisa nchini Libya wa kile alichokiita Khalef " uingiliaji kati wa vigogo" pia hakuzaa matokeo ya kutia moyo.
Amesema tajiriba hiyo mbaya imewafanya viongozi wengi na hasa Rais Obama kuwa na mashaka makubwa linapokuja suala la kuingilia kati kijeshi.Syria imeonya kwamba itapambana na vikosi vyoyote vile vitakavyopelekwa nchini mwake bila ya kibali chake.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP/dpa
Mhariri : Saumu Yusuf