1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahala juu ya Uislamu katika Ujerumani

13 Januari 2011

Kuna dhana nyingi zinazonasibishwa na Uislamu nchini Ujerumani. Hivi jee , ni kweli kuwa Ujerumani pia ni nyumbani kwa Waislamu, licha ya kuishi nchini humo karibu Waislamu milioni nne?

https://p.dw.com/p/zxBe
Hakuna matatizo: Uislamu uko nyumbani UjerumaniPicha: picture alliance / dpa

Mada zimepangwa vyema, kutoka ile yenye utata ihusuyo elimu ya uimamu nchini Ujerumani hadi utamaduni wa Kiislamu, hadi wanahabari wa Kijerumani wenye asili ya wahamiaji na maana ya Uislamu katika mazingira halisi ya kisiasa. Kiasi ya waandishi 50 wamegaiwa kuandikia masuala haya, na hakujakuwa na tatizo la nani atashinda kwenye mradi huu, kama anavyosema Mkuu wa Mabaraza ya Utamaduni ya Ujerumani, Olaf Zimmermann:

Imam Islam Freitagsgebet Moschee Duisburg Deutschland Religion
Mwanachuoni was Kiislamu akitoa mawaidha msikitiniPicha: picture alliance/dpa

"Kuna maulamaa wengi wa Uislamu, ambao wenyewe ni Waislamu, na ambao wamekuja, lakini pia kuna mtu kama rais wa idara ya Katiba ya Ujerumani naye pia ameandika kwenye muswaada huu. Kwetu sisi ni muhimu kuionesha picha halisi."

Maelezo haya yanahitajika sana, anasema pia Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu la Ujerumani, Aiman Mazyek. Tangu mashambulizi ya Septemba 11, 2001, wakosoaji wa Uislamu wamekuwa haweshi kuupa Uislam majina mabaya kama ilivyotokea kwa mwanasiasa wa chama cha SPD, Thilo Sarrazin, ambaye alizungumzia hatari ya Ujerumani kugeuzwa kuwa jamii ya Kiislamu. Lakini haifahamiki ni kwa vipi isionekane kuwa jamii inaweza kufaidika na kuwapo kwa Uislamu hapa:

"Tunaishi kwenye jamii inayojikuta kwenye mageuzi makubwa. Tunaishi pia na jamii za iliyokuwa kambi ya mashariki, ambazo zina malezi tafauti. Tunaishi pia kwenye wakati ambao tunashuhudia maendeleo ya kiuchumi. Na tunaishi pia katika wakati ambao lazima tuwe wawazi kwamba Uislamu ni sehemu ya picha hiyo yote."

Wulff: "Uislamu uko nyumbani Ujerumani"

Kauli kwamba Ujerumani pia ni nyumbani pa Uislamu ilitolewa na Rais wa Ujerumani, Christian Wulff, tarehe 3 Oktoba, mwaka jana katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 20 ya Muungano wa Ujerumani, na tangu hapo si katika chama chake tu mwangwi wa sauti hii ulikosambaa.

Christian Wulff
Rais Christian WulffPicha: picture alliance / dpa

Kiasi ya Waislam milioni nne wanaoishi hapa, tayari Ujerumani ndipo nyumbani pao. Lakini vipi kuhusu Uislamu wenyewe? Hilo ndilo suala ambalo linaulizwa na Baraza la Utamaduni la Ujerumani. Hilo ni jambo kubwa kwenye mada ya ujumuishaji wa wageni katika jamii ya Kijerumani, ambalo halijapatiwa majibu ya kutosha:

"Hilo ni jambo ambalo pia limeangaliwa kwa uchache sana na wasomi. Na kwa hilo nina hakika kuwa muswaada huu utakuwa na mijadala na midahalo ya kutosha. Natarajia bado hatujachelewa."

Baraza la Utamaduni la Ujerumani linataka pia kuhakikisha kuwa hisia za watu kuhusu Uislamu zinapewa nafasi yake. Waraka pekee ambao tayari umeshachapishwa kwa msaada wa Wakfu wa Robert Bosch, unaweza kupatikana bure.

Lengo la mradi huu ni kuwa na maandiko ya kutosha kuhusu taswira ya Waislamu na Uislamu nchini Ujerumani, kusudi watu wanapojadili maisha na hatima ya jamii ya Kiislamu ndani ya Ujerumani, wawe na maarifa ya kutosha kuhusu mada hiyo.

Mwandishi: Slike Bartlick/ZPR/Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman