McCarthy aapa kusalia katika mbio za uspika Marekani
4 Januari 2023Katika siku ya kwanza ya kile kinachodhihirisha kuwepo mapambano makali chamani kati ya wanachama 20 wa msimamo mkali na wajumbe wengine 202 wa Republican, McCarthy alishindwa katika duru tatu za upigaji kura kupata kura 218 aliohitaji kuwa spika, wadhifa ambao ni wa pili kuingia Ikulu ya White House baada ya Makamu wa rais.
Soma pia: Wabunge Marekani kumchagua spika mpya
Ulikuwa mwanzo wa kutatanisha kwa Warepublican ambao wana wingi mchache na unaangazia changamoto ambazo chama hicho huenda zikakabiliana nazo katika miaka miwili ijayo, kueleeka katika uchaguzi war ais wa 2024. Wingi wao mchache wa viti 222 dhidi ya 212 unaupa nguvu kubwa kundi dogo la wajumbe wa msimamo mkali, wanaotaka mabadiliko ya kanuni yanayoweza kuwapa udhibiti dhidi ya spika na ushawishi kuhusu mbinu ya chama hicho kwenye matumizi na madeni.
McCarthy amewaambia waandishi Habari kuwa rais wa zamani Donald Trump alimpigia simu na kusisitiza kumuunga mkono.
Trump anamuunga mkono McCarthy katika kinyang'anyiro hicho na bado ni kiongozi mwenye nguvu katika chama cha Republican.
McCarthy mwenye umri wa miaka 57 kutoka California, alijua kuwa anakabiliwa na mlima mkubwa wa kupanda kuelekea katika uchaguzi wa jana na alikuwa ameapa kuendelea kupambana. Lakini bunge lilipiga kura jana kuahirisha vikao hadi leo mchana, hatua ambayo itawapa Warepublican muda wa kujadili wagombea wengine. Mbunge wa kihafishina Jim Jordan, mwenye umri wa miaka 58 kutoka Ohio, alishinda kura 20 katika duru ya mwisho ya upigaji kura jana, ikiwa ni chini Zaidi ya kura zinazohitajika 218 kuwa spika, lakini zilitosha kumzuia McCarthy.
Mkwamo huenda ukavuruga shughuli za bunge kwa kiasi kikubwa na huenda ukawalazimu wabunge kuzingatia mgombea mwingine Mrepublican. Kiongozi mtarajiwa wa Warepublican bungeni Steve Scalise mwenye umri wa miaka 57 kutoka Louisiana, anaonekana kuwa chaguo. Mara ya mwisho bunge lilishindwa kumchagua spika katika duru ya kwanza ilikuwa mwaka wa 1923
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters