1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUhispania

Mbappe atambulishwa kama mchezaji wa Real Madrid

16 Julai 2024

Nyota wa kandanda wa Ufaransa Kylian Mbappe ametambulishwa rasmi kama mchezaji wa Real Madrid. Hafla hiyo imefanyika katika dimba la Santiago Bernabeu lililofurika mashabiki 80,000.

https://p.dw.com/p/4iNNo
Kylian Mbappe atambulishwa Madrid
Mbappe amesaini mkataba wa miaka mitano na atavaa jezi nambari 9Picha: Isabel Infantes/empics/picture alliance

Kylian Mbappe hatimaye amevaa jezi ya Real Madrid na kutimiza ndoto yake ya tangu utotoni mbele ya mashabiki waliofurika katika dimba la Santiago Bernabeu.

Karibu mashabiki 80,000 walifika Bernabeu kumkaribisha nyota huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 25 wakati wa hafla ya kutambulishwa kwake kama mchezaji wao mpya kabisa.

Soma pia: Mbappe kucheza mechi yake ya mwisho akiwa na PSG mjini Paris

Baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano na miamba hao wa Uhispania akiwa pembeni ya rais Florentino Perez, Mbappe alipanda jukwaani katika dimba la Bernabeu na kukaribishwa kwa shangwe na vifijo.

Akiwa amepigilia jezi nambari 9 Mbappe alitabasamu na kuwapungia mkono mashabiki walioimba jina lake, kisha akamkumbatia Perez na mchezaji wa zamani wa Madrid na kocha Zinedine Zidane, aliyemualika Mbappe kuitembelea klabu hiyo ya Uhispania kwa mara ya kwanza wakati akiwa kijana mdogo. Mbappe alizungumza katika Kihispania akisema.

"Kwa miaka mingi, nimekuwa na ndoto ya kuichezea Real Madrid na leo ndoto yangu imetimia. Ntajitolea Maisha yangu kwa ajili ya klabu hii”.