1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kati ya jeshi na wanamgambo wa Sudan yaanza

11 Julai 2024

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya wanamgambo wa RSF yameanza Geneva, Uswisi, huku Shirika la Msalaba Mwekundu likisema kwamba sehemu kubwa ya Sudan haiwezi kufikiwa na misaada.

https://p.dw.com/p/4i9lb
Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan (RSF) vinaandamana wakati wa uzinduzi huko Khartoum, Sudan, Mei 13, 2017.
Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan (RSF) vinaandamana wakati wa uzinduzi huko Khartoum, Sudan, Mei 13, 2017.Picha: Mohamed Babiker/Photoshot/picture alliance

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya wanamgambo wa (RSF) yameanza Geneva, Uswisi, yakituama juu ya masuala ya misaada ya kibinadamu.

Haya yanajiri huku shirika la msalaba mwekundu likitangaza kwamba sehemu kubwa ya Sudan iliyokumbwa na vita haiwezi kufikiwa na wafanyakazi wa misaada ya kiutu.

Tovuti binafsi ya habari ya Rakoba ya nchini Sudan, imeripoti Alhamisi kwamba "mikutano isiyo ya moja kwa moja imeanza Jumatano mjini Geneva, Uswisi, kati ya wawakilishi wa serikali ya Sudan na vikosi vya RSF, kujadili masuala ya kibinadamu".

Imenukuu gazeti la Al-Quds al-Araby lenye makao yake mjini London likisema kuwa "mikutano hiyo ilitanguliwa na mashauriano ambayo hayajatangazwa na pande za Sudan, ambayo yalidumu kwa wiki kadhaa ili kupiga jeki majadiliano kati ya jeshi la Sudan na RSF, yakilenga kuzingatia mgogoro wa kibinadamu unaoshuhudiwa nchini Sudan na juhudi za kusitisha mapigano".

Juhudi za mazungumzo kati ya jeshi la Sudan na RSF

Haya yanaibuka huku kukiwa na msukumo mpya wa Saudi Arabia kuanza tena mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili, ambayo yangefanyika mjini Jeddah.

Pia yanakuja siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kutembelea Bandari ya Sudan na kujadili mzozo wa Sudan na kiongozi wa nchi hiyo na mkuu wa jeshi, Abdel Fattah al-Burhan.

Soma zaidi: Changamoto mpya kwa wakimbizi wa Sudan nchini Chad

Kulingana na Umoja wa Mataifa  mzozo huo umesababisha maelfu ya watu kuuawa na kuwafurusha zaidi ya watu milioni kumi.

Pierre Dorbes, mwakilishi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) amesema "Kuna maeneo mengi ambayo hawawezi kuyafikia, wakati mwingine kwa sababu ni hatari sana, na wakati mwingine hawapati ruhusa."

Watu wanapanga foleni kujiandikisha kwa ajili ya utoaji wa msaada wa chakula katika kambi ya wakimbizi wa ndani (IDP) huko Agari, Kordofan Kusini, Juni 17, 2024.
Watu wanapanga foleni kujiandikisha kwa ajili ya utoaji wa msaada wa chakula katika kambi ya wakimbizi wa ndani (IDP) huko Agari, Kordofan Kusini, Juni 17, 2024.Picha: Guy Peterson/AFP

Dorbes anasema kuboresha ufikiaji kutasaidia mamilioni ya watu. Aliyasema haya kwenye kikao na waandishi wa habari huko Port Sudan, mji ulio karibu na Bahari Nyekundu ambapo jeshi, serikali na mashirika ya Umoja wa Mataifa sasa ndiyo yamepiga kambi.

Mzozo wa kivita umeshuhudiwa nchini Sudan tangu Aprili 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo chini ya Abdel Fattah al-Burhan na vikosi vya RSF, vinavyoongozwa na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.

Vituo vya kuwapikia watu chakula vyaanzishwa 

Ripoti ya hivi majuzi inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilisema karibu watu milioni 26, au zaidi ya nusu ya watu, wanakabiliwa na viwango vya juu vya "uhaba mkubwa wa chakula".

Makundi ya kujitolea katika baadhi ya maeneo ambako kuna vurugu kubwa yameanzisha vituo vya kuwapikia watu chakula, vikisaidiwa na mashirika ya kimataifa kutoa chakula kwa waathiriwa.

Soma zaidi: UN: Sudan yakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

Esmat Mohamed, ambaye anasimamia mpango mmoja kama huo katika mji mkuu Khartoum, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanatoa "takriban milo 2,000 kwa siku, na idadi hiyo inaongezeka kila siku".

Lakini mfanyakazi mmoja aliyeomba kutotajwa jina kwa sababu za usalama amesema makundi ya kimataifa yanakabiliwa na vizingiti ikiwemo uwezo wa kuwatumia fedha wafanyakazi wa kujitolea wanatoa misaada kwa wahanga wa machafuko. 

Katika mji wa Dilling, karibu na mpaka wa Sudan Kusini, Kinda Komi ni mmoja wa watu waliojitolea kutoa chakula kwa wale wanaohitaji.

Anasema, "tangu kuanza kwa vita, hakuna msaada wa chakula umefika katika mji huo, na barabara zinazouunganisha na nchi nzima zimekatwa kutokana na mapigano". Kulingana naye, "nusu ya wale wanaohitaji huondoka bila kupokea chakula."