Mazungumzo ya Syria yamalizika bila mafanikio
1 Februari 2014Hakuna makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa wakati mazungumzo hayo yakifikia mwisho jana Ijumaa(31.01.2014),mazungumzo kuhusu kuundwa kwa serikali ya mpito hayakuanza , na makubaliano ya kuruhusu misaada kuingia katika maeneo yaliyozingirwa yanayodhibitiwa na waasi katika mji wa kati wa Homs hayakufika popote.
Wingu limetanda zaidi baada ya shirika linaloangalia haki za binadaamu nchini Syria kusema kuwa karibu watu 1,900 wameuwawa tangu mazungumzo hayo yaanze wiki moja iliyopita.
Marekani pia imemuonya Rais wa Syria Bashar al-Assad kuwa atawajibishwa kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya kimataifa ya kuondoa hazina ya silaha za sumu nchini humo.
Mvutano bado waendelea
Mjini Geneva , wiki ya majadiliano ya faragha ilimalizika kwa pande zinazopingana kuendelea kuvutana kuhusiana na nani anabeba lawama katika mzozo huo uliosababisha umwagikaji mkubwa wa damu ambao umesababisha zaidi ya watu 130,000 kupoteza maisha.
Mpatanishi wa Umoja wa mataifa na nchi za kiarabu Lakhdar Brahimi , ambaye amefanikisha kuzikutanisha pande hizo mbili katika mkutano kwa mara ya kwanza tangu mzozo huo kuanza Machi mwaka 2011, amesema analenga kuitisha tena duru nyingine ya mazungumzo kuanzia Februari 10.
Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Syria Walid Muallem amesema hakuna matokeo sahihi yanayoonekana kutoka katika mazungumzo hayo ya Geneva , na kwamba Assad na serikali yake watatafakari iwapo kuna maana yoyote kurejea kwa duru ya pili.
Matamshi hayo yalizusha ukosoaji kutoka kwa mshirika mkuu wa upinzani Marekani."Utawala unaendelea kufanya mchezo," msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Edgar Vasquez amesema.
Mkuu wa kundi la upinzani Ahmad Jarba amethibitisha kuwa upinzani utarejea ,hata kama kukaa pamoja na utawala kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita ilikuwa ni kama, "kunywa kitu kilichotiwa sumu katika kibuyu".
Lakini amesisitiza kwamba kuwapo kwao ilikuwa kwa masharti ya kupatiwa ,"uwezo wa kuwahami watu wetu katika vita."
"Kasi ya kuunga mkono mapinduzi inaongezeka haraka, kama unavyosikia hivi karibuni," amesema.
Ripoti za vyombo vya habari ambazo hazikuthibitishwa wiki hii zimedai kuwa bunge la Marekani hivi karibuni limeidhinisha kuanza tena kuwapa waasi silaha, kwa makundi ya waasi yenye msimamo wa wastani nchini Syria.
Urusi kuzungumza na upinzani
Akishughulikia kuungwa mkono, Jarba anatarajiwa kufanya ziara nchini Urusi siku ya Jumanne, nchi ambayo ni mshirika mkuu wa Assad katika safu ya kimataifa.
Afisa mwandamizi wa Marekani amesifu ziara hiyo inayopangwa , akisisitiza kuwa inaonesha "upande wa Urusi unatambua kuwa kundi la upinzani la muungano wa kitaifa pia unajukumu katika kutatua mzozo wa Syria."
Brahimi amezitaka Marekani na Urusi , ambazo zimehangaika kwa muda wa miezi minane kuzileta pamoja pande zinazopigana katika meza ya majadiliano, pamoja na wengine kuweza kutumia ushawishi wao kumaliza mauaji nchini Syria.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amewaambia waandishi habari kabla ya mazungumzo yake mjini Berlin na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kuwa serikali ya Syria haitekelezi muda uliokubaliawa kati ya Marekani na Urusi wa kusafirisha nje hazina yake ya silaha za sumu.
Amesema vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo "vinasababisha hali ya kutokuwa na uthabiti katika eneo lote".
Baadaye Kerry alikutana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov pembezoni mwa mkutano wa usalama mjini Munich , ambapo Syria ilikuwa mada kuu.
Mpatanishi wa kimataifa Lakhdar Brahimi ameyataka mataifa makubwa duniani kuweka mbinyo dhidi ya serikali ya Syria na upinzani kufanya mazungumzo ya maana juu ya kumaliza mzozo huo wakati watakapokutana tena kwa duru ya pili ya mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / afpe
Mhariri: Caro Robi