Mazungumzo ya Syria yaanza kwa mashaka
23 Januari 2017Mjumbe wa serikali ya Syria kwenye mazungumzo hayo, amesema kauli zinazotolewa na mkuu wa makundi ya upinzani ni za uchokozi na zisizokwendana na uhalisia.
Bashar Ja'afari, ambaye pia ni balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, amewaambia waandishi wa habari nje ya jengo la mikutano mjini Astana kwamba hotuba ya Mohammad Alloush haikuwa na hadhi ya kutolewa mbele ya wanadiplomasia wa hadhi ya juu wanaokutana hapo
"Kauli zenye mahadhi ya uchokozi na majigambo za mkuu wa ujumbe wa magaidi zilikuwa matusi kwa jopo la wanadiplomasia waliopo hapa. Ni kuisoma visivyo hali ya Syria na kauli za uthubutu usio maana unaoakisi namna wasivyojuwa kile walichokisaini;" alisema Ja'afari.
Awali mkuu wa ujumbe wa makundi ya upinzani, Alloush, alisema kwamba kabla ya kusonga mbele kwenye majadiliano, ni sharti usitishaji mapigano uliokubaliwa uthibitike kuwa unaheshimiwa kwenyewe nchini Syria, akisisitiza pia kuwa kwao wao ni muhimu kurejeshwa kwa misaada ya kibinaadamu wakati huu mazugumzo yakiendelea.
"Hatua ya kwanza ni kuhakikisha usitishaji mapigano na makubaliano ya Disemba 30. Tutakapokuwa na hakika kuwa usitishaji huu wa mapigano ni wa kweli huko kwenye mapigano yenyewe, hapo ndipo tunapoweza kuelekea kwenye hatua nyengine, ambazo tunaweza kuziadili kwenye duru nyengine ya mazungumzo," alisema Alloush.
Upinzani watishia kuendelea na mapigano
Hayo yakiendelea, makundi mengine ya waasi yameapa kuendelea na mapigano endapo mazungumzo haya yatashindwa. Msemaji wa waasi, Osama Abu Zeid, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hawatakuwa na uchaguzi mwengine ila vita.
Tangazo hili la waasi linakuja huku wizara ya ulinzi ya Urusi ikisema kwamba ndege zake za kivita ziliyashambulia maeneo yanayoshikiliwa na kundi lijitalo Dola la Kiislamu, karibu na mji wa Deir Ezzor, mashariki mwa Syria, kwahala ambako majeshi ya serikali yamekuwa pia yakipigana na waasi.
Msemaji wa kundi jengine la waasi, Yahya al-Aridi, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba upinzani ulijitoa kwenye duru ya kwanza ya mazungumzo ya moja kwa moja mjini Astana, kwa sababu serikali ilikuwa inaendelea kuyashambulia maeneo yaliyo karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus.
Duru kadhaa za mazungumzo kama haya zimewahi kushindwa kufikia suluhu huko nyuma mjini Geneva na New York yakiwa yanahudhuriwa zaidi na wasiasa wakubwa wa Syria, ingawa haya ya sasa yanaonekana kuwashirikisha wanachama wa makundi yenye silaha, huku wale wa wapinzani wa kisiasa wakiwa kama washauri tu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman