1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia yaingia duru ya tatu

22 Novemba 2013

Mazungumzo muhimu kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kati ya nchi hiyo na mataifa makubwa duniani yanaingia siku ya tatu Ijumaa (22.11.2011) ambayo ni ya hatua ya kufa na kupona wakati hakuna maendeleo makubwa yaliofikiwa.

https://p.dw.com/p/1AMLv
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja Ulaya Catherine Ashton (kushoto) akizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya nuklea ya siku tatu mjini Geneva.(20.11.2013).
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja Ulaya Catherine Ashton (kushoto) akizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya nyuklia ya siku tatu mjini Geneva.(20.11.2013).Picha: Reuters

Duru hiyo ya tatu ya mazungumzo mjini Geneva tokea Rais Hassan Rouhani wa Iran achaguliwe kushika wadhifa huo hapo mwezi wa Juni inatowa matumani makubwa kuwahi kushuhudiwa kwa miaka mingi katika kuutafutia ufumbuzi mzozo uliodumu kwa muongo mmoja wa mpango wa nyuklia wa Iran.

Hata hivyo ni kazi pevu kufikia makubalino yatakayoweza kuwatuliza wanasiasa wa misimamo mikali wenye mashaka nchini Marekani na katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Israel.Wanadiplomasia kadhaa wa mataifa ya magharibi wanasema kuna uwezekano mkubwa kwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kujiunga na mataifa mengine makubwa sita mjini Geneva katika jaribio jengine la kufikia makubaliano na Iran.

Yumkini mazungumzo kuendelea Jumamosi

Hata hivyo mwanadiplomasia mmoja mwandamizi amewaambia waandishi wa habari kwamba mawaziri hao watakwenda tu Geneva iwapo kutakuwa na makubaliano ya kutiwa saini.Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo kuna maendeleo fulani yaliofikiwa yakiwemo masuala muhimu lakini kuna mambo manne mapaka matano hivi yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi.Ameongeza kusema kuna mambo ambayo Iran imeyapendekeza ambayo yanakubalika na kuna mambo ambayo hayakubaliki. Pia ameongeza kusema kwamba hakuna mtu anayependekeza kwamba mazungumzo hayo yanapaswa kuvunjwa na amedokeza yumkini yakaendelea hadi Jumamosi.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araqchi akitilia mkazo kauli ya mwanadiplomasia huyo wa mataifa ya magharibi amesema bado wana maoni tafauti juu ya baadhi ya vipengele na hadi hapo watakapokuwa karibu kuvipatia ufumbuzi mawaziri hao wa mambo ya nje hawatokwenda Geneva.

Mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa mjini Geneva.(20.11.2013).
Mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa mjini Geneva.(20.11.2013).Picha: Reuters

Kile kinachojadiliwa ni usitishaji wa Iran wa sehemu ya shughuli zake nyeti za nyuklia hasa zile za kurutubuisha madini ya urani ya kiwango cha wastani ili nchi hiyo ipate kuregezewa vikwazo,kutakakojumuisha kuachiliwa kwa baadhi ya fedha za Iran zinazozuiliwa katika mabenki ya kigeni na kuruhusu biashara yake yakiwemo mafuta.

Shinikizo lingalipo

Nchini Marekani kuna shinikizo la wabunge wa nchi hiyo kupuuza wito wa Rais Barack Obama na kuidhinisha vikwazo zaidi dhidi ya Iran iwapo hakuna makubaliano yatakayofikiwa au makubaliano yatakayofikiwa yataonekana kuwa dhaifu sana.

Kiongozi wa baraza la Seneti wa chama cha Demokratik Harry Reid.
Kiongozi wa baraza la Seneti wa chama cha Demokratik Harry Reid.Picha: Reuters

Akiongezea shinikizo hilo kiongozi wa chama cha Demokratik chenye wingi wa viti katika baraza la Seneti la bunge la Marekani Harry Reid amesema mjini Washington hapo jana kwamba wabunge watachukuwa hatua ya kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran hapo mwezi wa Disemba.

Rais wa Iran Hassan Rouhani naye pia yuko katika shinikizo kumuonyesha kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei matunda ya kwanza ya "haiba yake ya uchangamfu " na haiko wazi iwapo pendekezo la kuregezewa vikwazo kwa nchi hiyo litakidhi haja.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu