1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Montreux yawiva

17 Januari 2014

Matayarisho ya mkutano wa wiki ijayo mjini Montreux kusaka amani ya Syria yanaelezwa kufikia hatua nzuri, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje Walid Mualle ametangaza mpango wa kubadilishana wafungwa na waasi.

https://p.dw.com/p/1AsZb
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid Muallem (kushoto), na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow siku ya Ijumaa, tarehe 17 Januari 2014.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid Muallem (kushoto), na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow siku ya Ijumaa, tarehe 17 Januari 2014.Picha: AP

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kati yake na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, mjini Moscow hivi leo, Muallem amesema ameikabidhi serikali ya Urusi mipango ya usitishaji mapigano katika mji mkubwa zaidi nchini Syria, Aleppo, na kwamba serikali yake iko tayari kubadilishana orodha na makundi ya waasi juu ya uwezekano wa kubadilishana wafungwa.

Kwa mujibu wa Sergei Lavrov, wawakilishi wa serikali na upinzani wa Syria watakutana uso kwa uso zaidi ya mara moja kwenye mkutano wa kusaka amani wiki ijayo mjini Montreaux.

Lavrov amekataa kutaja kwa uhakika ni mara ngapi hasa wawakilishi hao watakapokutana, lakini amesema ana hakika mkutano hautamalizika tarehe 22 Januari, bali utakuwa ndio umeanza.

Makundi ya upinzani ya Syria, ambayo yamekuwa yakishindwa kuwa na msimamo wa pamoja, yanakutana leo mjini Istanbul, Uturuki, kuamua ikiwa yashiriki kwenye mazungumzo hayo, huku washirika wao wa Kiarabu na Kimagharibi wakiwashinikiza kuhudhuria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amewatolea wito wapinzani wa Assad kutoa uamuzi muafaka wa kuwa sehemu ya mazungumzo.

"Tunajua kuwa mkutano wa amani wa Geneva sio mwisho, bali mwanzo, ni uzinduzi wa mchakato, mchakato ambao ni fursa bora kabisa kwa upinzani kufikia malengo ya watu wa Syria na mapinduzi na suluhisho la kisiasa kwa mgogoro huu wa mbaya kabisa ambao umeshateketeza maisha ya watu wengi, wengi sana kabisa." Alisema Kerry.

Ushiriki wa Iran

Suala muhimu katika matayarisho ya mkutano huo, limekuwa ushiriki wa Iran, ambapo Urusi inashikilia lazima Iran iwemo, huku mataifa ya Magharibi yakiishutumu nchi hiyo kuusaidia kijeshi utawala wa Assad, na pia kuliunga mkono kundi la Hizbullah nchini Lebanon, ambalo linapigana upande wa Assad nchini Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (kulia) na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow siku ya Alhamisi, tarehe 16 Januari 2014.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (kulia) na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow siku ya Alhamisi, tarehe 16 Januari 2014.Picha: Mehr

Marekani inataka kabla ya kuruhusiwa kushiriki kwenye mkutano huo, kwanza Iran iunge mkono waziwazi malengo ya mkutano huo, likiwemo la kuanzishwa kwa serikali ya mpito nchini Syria.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Moscow hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, alisema nchi yake haitakubali masharti yoyote katika kuhudhuria mkutano huo.

Mnamo mwezi Juni 2012, Marekani na Urusi zilikubaliana mjini Geneva juu ya utaratibu wa kupatikana kwa amani nchini Syria, unaojumuisha kukabidhiwa madaraka kwa chombo ambacho kitakuwa na mamlaka ya kiutendaji.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Josephat Charo