1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa kuunda serikali mpya Ujerumani yamekwama

5 Novemba 2021

Juhudi za vyama vya Ujerumani za kuunda serikali mpya ya muungano na kupatikana kansela mpya atakaechukua mikoba ya Angela Merkel zinakabiliana na changamoto.

https://p.dw.com/p/42drN
PK nach Ampel-Sondierungsgesprächen
Picha: CHRISTOF STACHE/AFP

Uwekezaji katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, mustakabali wa sekta ya viwanda vya magari na nani atakayeshikilia nafasi ya waziri wa fedha, atakayekuwa na nafasi muhimu ya kuuongoza uchumi wa Ulaya ni mambo yanayoleta mkwamo katika kufikia makubaliano hayo.

Naibu kiongozi wa chama cha Kijani Robert Habeck pamoja na kiongozi wa chama cha kiliberali FDP Christian Lindner, wote wanang'ang'ania nafasi hiyo na hakuna aliyekuwa tayari kuiachia, licha ya muda wa mwisho wa kufikia makubaliano hayo kukaribia.

Mwanachama mkongwe wa FDP Wolfgang Kubicki amesema kufuatia chama hicho kujulikana kama chama chenye nidhamu, kupewa nafasi yoyote isipokuwa nafasi ya waziri wa fedha ni fedheha.

Soma zaidi: Ujerumani: Scholz akubaliana na Kijani, FDP kuanza mazungumzo ya kuunda serikali

Tatizo kubwa linaloleta mkwamo kwa chama cha Kijani ni mipango ya ulinzi wa mazingira, chama hicho kinataka kitita cha euro bilioni 50 kila mwaka katika uwekezaji wa suala hilo.

Chama hicho kimependekeza mipango mipya ya ukopaji na kupandishwa kwa ushuru kwa wale wanaopokea kiwango cha juu cha mshahara, kulipia masharti yaliyowekwa wanayosema ni muhimu kwa mustakabali wa siku za usoni wa Ujerumani. Hata hivyo kiongozi wa chama kinachoegemea biashara FDP ameonekana kupinga mapendekezo ya chama cha Kijani.

Deutschland Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/C. Koall

Ahadi za wakati wa kampeni zarudisha nyuma mazungumzo

Kulingana na gazeti la kila siku la Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung, ni changamoto kwa vyama hivyo vitatu kuungana kutokana na sera zao na ahadi zao kwa wapiga kura wakati wa kampeni ambazo kila mmoja angelitaka kuzitimiza.

Kufuatia kushindwa vibaya kwa chama cha kihafidhina cha CDU cha Kansela wa Ujerumani anayeondoka Angela Merkel, katika uchaguzi uliofanyika mwezi Septemba, chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto SPD na kiongozi wake Olaf Scholz kilipata nafasi ya kuunda serikali mpya ya Muungano.

Soma zaidi:Ujerumani: Mazungumzo ya kuunda serikali yafikia pazuri

Lakini mazungumzo hayo na chama cha Kijani kinachotetea ulinzi wa mazingira pamoja na kile cha kiliberali cha FDP yalionekana kuendelea vizuri mwezi Oktoba, ingawa kwa sasa yamechukua mkondo tofauti. Iwapo vyama hivyo havitajaribu kutafuta mbinu ya pamoja ya kuunda serikali hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba matumaini ya kumuona Scholz akiapishwa kama kansela mpya Desemba 6, huenda yakacheleweshwa.

Kiongozi wa chama cha Kijani Annalena Baerbock amesema hawezi kusema ni lini watakapokubaliana kuunda serikali maana bado kuna masuala muhimu yanayohitaji kufikiwa.