Pande zinazozana Yemen kubadilishana wafungwa
16 Desemba 2015Leo pande hizo zimekubaliana kubadilishana mamia ya wafungwa kama sehemu ya kujenga imani miongoni mwao katika meza ya mazungumzo.
Afisa mwandamizi wa kikiosi cha wapiganaji walio watiifu kwa Rais Hadi Abdel Hakim al Hasani amesema waasi 360 wa Houthi wanaouzuiwa mjini Aden wataachiwa huru na raia 265 na wapiganaji kutoka kusini mwa Yemen wataachiwa pia leo mchana kupitia upatanishi wa kikabila.
Pande zinazozana kubadilishana wafungwa
Afisa anayesimamia gereza la waasi wa Houthi katika mji wa Sanaa amesema wafungwa hao tayari wameshaabiri mabasi kuelekea katika eneo ambalo watabadilishana wafungwa katika mpaka unaogowanya kaskazini na kusini mwa Yemen.
Inaripotiwa pia mabasi yameonekeana yakiondoka mji wa Aden yakisindikizwa na wapiganaji kuelekea katika eneo hilo la kubadilishana wafungwa.
Mazungumzo hayo yanayoileta serikali ya Yemen inayotambulika na jumuiya ya kimataifa na waasi wa kishia wa Houthi yalianza jana na yanalenga kuzipa pande hizo mbili fursa ya kuutafutia ufumbuzi mzozo uliokumba Yemen ambayo ndiyo nchi maskini zaidi ya kiarabu.
Maafisa wa usalama hata hivyo wameripoti kuwa waasi wamekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku saba kama sehemu ya kuyandaa mazingira muafaka ya kufanyika mazungumzo hayo ya amani.
Mapigano yameripotiwa katika jimbo la Taez na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulijibu mashambulizi hayo ya waasi kwa kufanya mashambulizi kadhaa ya angani jana nzima.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed amesisitiza umuhimu wa kufanyika mazungumzo hayo ya Geneva kwani watu wa Yemen wanatarajia matokeo ya kutia moyo kutoka kwa duru hiyo ya mazungumzo.
Ould Cheikh ameongeza kuwa mazungunzo hayo kati ya serikali na waasi ndiyo tumaini la pekee kwa raia wa Yemen na matumaini hayo hayapaswi kuzimwa.
Je duru mpya ya mazungumzo itafanikiwa?
Juhudi za kipindi cha nyuma za kuutafutia ufumbuzi mzozo huo wa Yemen hazikufua dafu. Serikali ya Yemen inaoyoongozwa na Rais Abed Rabbo Mansour Hadi imekuwa ikisisitiza waasi wa Houthi wasalimishe silaha na kuondoka kutoka maeneo wanayoyadhibiti ikiwemo katika mji mkuu wa Yemen Sanaa, kuambatana na azimio la Umoja wa Mataifa.
Waasi wa Houthi kwa upande wao wanataka hatma ya kisiasa ya taifa hilo iamuliwe kupitia mashauriano. Wakati wa kipindi cha kusitisha mapigano, pande zote mbili zimekubaliana kuruhusu kusafirishwa kwa misaada ya kibinadamu bila ya masharti.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Ahmed Fawzi amesema washiriki wa mazungumzo hayo wametia saini makubaliano ya kuahidi kutozungumza na vyombo vya habari hadi watakapokamilisha mazungumzo hayo ambayo huenda yakadumu kwa siku kadhaa.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, vita hivyo vya Yemen vimesababisha vifo vya takriban watu 5,800 tangu mwezi Machi mwaka huu.
Mwandishi: Caro Robi/ap/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman