1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kutafuta amani Syria yaanza Geneva

Caro Robi
28 Novemba 2017

Duru ya nane ya mazungumzo ya kutafuta amani Syria imeanza Geneva lakini tangazo la dakika za mwisho la Serikali ya Syria kuwa huenda isitume wajumbe ni pigo kwa juhudi za kutafuta suluhisho kwa mzozo wa Syria.

https://p.dw.com/p/2oN45
Schweiz Syrien-Friedengsgespräche in Genf
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Duru hii ya mazungumzo ilionekana kama fursa ya mwisho ya Umoja wa Mataifa kusogesha mbele juhudi za kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu, kuwaacha mamilioni bila ya makazi na kuharibu vibaya miundo mbinu Syria.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura amesisitiza kuna haja ya kupatikana kwa dharura suluhisho la kisiasa. Upande wa upinzani kwa mara ya kwanza unatuma ujumbe wa pamoja katika mazungumzo hayo.

Serikali haijatuma wajumbe

Hapo Jumatatu, de Mistura aliliambia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa serikali ya Rais Bashar al Assad bado haijathibitisha kutuma ujumbe katika mazungumzo hayo.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura akizungumza Geneva
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de MisturaPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Hayo yanajiri huku Viongozi wa Marekani na Ufaransa wakisisitiza kuwa mazungumzo ya kutafuta amani Syria yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa ndiyo njia pekee ya kuamua mustakabali wa siku za usoni wa Syria.

Ikulu ya Rais wa Marekani imesema Rais Donald Trump na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron walizungumza kwa njia ya simu na kukubaliana kuwa mazungumzo yanayoanza leo mjini Geneva kuhusu Syria ndiyo njia pekee halali ya kufikia suluhisho la kisiasa Syria.

Tangu kuanza kwa mazungumzo kuhusu Syria yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa mjini Geneva mwaka 2014, utawala wa Syria umekuwa ukiwakilishwa na viongozi wa ngazi ya juu, miongoni mwao balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar al Jaafari.

Duru hii mpya ya mazungumzo inakuja wakati amabpo utawala wa Assad ukiwa umepata mafanikio katika mapambano dhidi ya wanaotaka kumng'oa madarakani na wanamgambo wenye itikadi kali, tangu jeshi la Urusi kuanzisha operesheni ya kijeshi kuusaidia utawala wa Assad mwaka 2015.

Upinzani wamtaka Assad aondoke madarakani

Serikali sasa inadhibiti asilimia 55 ya maeneo nchini humo. Upande wa Serikali umekuwa ukipuuzilia mbali wito wa upinzani wa kumtaka Rais Assad kuondoka madarakani ukisisitiza hatma ya kiongozi huyo inapaswa kuamuliwa na Wasyria wenyewe kupitia chaguzi na sio katika meza ya mazungumzo.

Rais wa Syria Bashar al Assad na wa Urusi Vladimir Putin wakifanya mazungumzo mjini Sochi Novemba 20,2017
Rais wa Syria Bashar al Assad na wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/Sputnik/M. Klimentyev

Ujumbe wa Serikali katika kipinidi cha nyuma umekataa kukaa meza moja na upinzani ukiwataja magaidi au kusema wamegawika vibaya kudai kuwakilisha upinzani. Kutokana na ufanisi dhidi ya wanamgambo na waasi katika mapambano, Serikali ya Syria inaonekana haina nia ya kufanya mazungumzo na upinzani.

Na Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim amesema mazungumzo yanayoongozwa na Urusi, Uturuki na Iran yanayofanyika Astana, yanakwenda sambamba na ya Umoja wa Mataifa yanayofanyika Geneva na hayakinzani wala kushindana, bali ni kusaidia kuweka misingi madhubuti ya kufikiwa suluhisho kwa mzozo wa Syria.

Rais wa Urusi Vladimir Putin pamoja na wa Iran Hassan Rouhani na wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wameongeza juhudi za kidiplomasia na kijeshi Syria katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni ikiwemo kufanya duru saba ya mazungumzo, Astana, nchini Kazakhstan. Wiki iliyopita, Rais Assad alifanya mazungumzo na Putin nchini Urusi kuhusu namna ya kupatikana amani Syria.

Mazungumzo ya Astana yamepiga hatua kwa kuundwa kwa maeneo manne Syria ambayo mapigano yamesitishwa huku mazungumzo ya Geneva yanayonuia kuvimaliza vita Syria yakionekana kusuasua.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/ap

Mhariri:Josephat Charo