1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Geneva yahitimishwa

3 Machi 2017

Wakati mazungumzo ya amani ya Syria yakikaribia kuhitimishwa jijini Geneva, hakujaonekana kuwepo kwa makubaliano yaliyoahidiwa ama kufikiwa.

https://p.dw.com/p/2Yc3h
Schweiz UN Friedensgespräche Syrien in Genf
Picha: picture-alliance/abaca/M. Yalcin

Hata hivyo hakuna upande uliojiondoa katika mazungumzo hayo na wote wamedai kupata ushindi mdogo.

Urusi ambayo inaonekana kuwa katikati imekutana na pande zote zinazokinzana pembezoni mwa mazungumzo hayo, na wanadiplomasia wa magharibi wanaotaraji mazungumzo hayo kukamilika baadae leo hii huku kukiwa na ajenda ya makubaliano na mpango wa kufanyika kwa mazungumzo mengine mjini Geneva baadae mwezi huu.

Katika siku nane za mazungumzo, pande zinazokinzana hazikuwahi kuzungumza ana kwa ana, lakini  wajumbe walijadili agenda hizo chini ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, Staffan de Mistura anayetaka kujadiliwa kwa katiba mpya, uchaguzi na kuundwa serikali mpya.

Wakati rasimu ikiwa bado haijamalizika upinzani ulikutana na de. Mistura ili kujihakikishia iwapo mchakato huo utazingatia hatua ya mpito wa kisiasa, wamesema wanadiplomasia wa Magharibi. Mwakilishi wa Serikali ya Syria, Bashar al-Ja'afari yeye anataka suala la vita dhidi ya ugaidi liingizwe kwenye agenda.

Schweiz Syriengespräche in Genf
Mwakilishi wa serikali ya Syria kwenye mazungumzo ya amani ya Geneva, Bashar al Ja'afariPicha: Reuters/P. Albouy

Kuna hatua zinazochukuliwa na pande zote, lakini ugumu ni kwamba upinzani unataka kuna na uhakika ni kwa namna gani suala la ugaidi litadhibitiwa na kwa mfumo upi, amesema mwanadiplomasia mmoja. Amesema makundi hayo kinzani yanahitaji kuhakikishiwa kwamba mpango huo hautaingiliwa na serikali na kuharibu mpango mzima wa mpito wa kisiasa. De Mistura atalazimika kuwahakikishia kwamba pande zote hakuna mtego.

Msuluhishi huyo mkongwe wa Umoja wa Mataifa, ameonya dhidi ya matarajio ya kimiujiza, hasa kwa kuwa utawala mpya wa rais wa Marekani Donald Trump haujaweka wazo nafasi yake katika usuluhishi wa mzozo huo, na labda hakutakuwa na nafasi hiyo kabisa.

De Mistura amekuwa akikutana kila siku na wawakilishi kutoka serikali ya Syria na makundi ya upinzani, ambao katika mazungumzo ya awamu iliyopita hawakukutana ana kwa ana, isipokuwa tu wakati wa ufunguzi wiki iliyopita.

Kulingana na chanzo kimoja cha habari, Jana usiku ikiwa ni wiki moja tangu kuanza kwa mazungumzo hayo yaliyotiliwa matumaini, De Mistura alifanya mazungumzo hadi saa tisa za alfajiri. 

Leo hii de Mistura alikutana kwa mara nyingine na pande zote na kufanya mkutano wa kufunga mazungumzo hayo na waandishi wa habari leo jioni, na kama sivyo angefanya mkutano huo kesho Jumamosi, hii ikiwa ni kulingana na chanzo kingine cha habari. 

Wigo wa mazungumzo hayo umekuwa finyu tangu zaidi ya mwaka uliopita, wakati ambapo De Mistura alipolazimika kusikiliza mahitaji ya kusitisha mapigani na kuwaachia wafungwa. Mpango tete wa kusitisha mapigano ulianza kutekelezwa tangu mwezi Desemba mwaka jana, na mazungumzo tofauti yaliyofanyika Kazakhstan, na kufadhiliwa na Urusi, Uturuki na Iran yalihusiana na masuala ya kijeshi.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/AFPE.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman