1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wasema lazima Rais Assad aondoke madarakani

Amina 22 Machi 2016

Mazungumzo ya amani ya Syria yamechukua mkondo mpya juu ya hatima ya rais Bashar al Assad huku wanamgambo wa Hezbollah wakiapa kupambana sambamba na vikosi vya serikali ili kuwashinda nguvu wanamgambo wa IS.

https://p.dw.com/p/1IHQI
Syrien UN-Vertreter Bashar Jaafari
Mjumbe wa serikali ya Syria mjini Geneva Bashar al-JaafariPicha: picture alliance / AA

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa kwaajili ya Syria Staffan de Mistura, amesema amejaribu kuipa shinikizo Syria kuweka wazi hatua yake juu ya suala la suluhu ya kisiasa, huku mazungumzo hayo ya amani yanayofanyika mjini Geneva Uswisi yakiingia wiki yake ya pili.

De Mistura amesema mjumbe anayeongoza majadiliano upande wa Syria Bashar al-Jaafari amemuambia ni mapema sana kuzungumzia jambo hilo, huku akiongeza kuwa mustakbal wa Assad na suala la suluhu la kisiasa ni mambo mawili tofauti. Bashar amesema rais Assad hahusiki kwa njia yoyote ile na mazungumzo yanayoendelea Geneva akisisitiza kuwa suala la rais huyo ni kitu kilichotolewa zamani katika ajenda ya mazungumzo.

Aidha hatma ya rais Bashar al Assad imekuwa kizingiti katika mazungumzo ya hivi karibuni yanayonuiwa kumaliza mapigano nchini humo yaliyoingia mwaka wake wa tano, na yaliyosababisha mauaji ya zaidi ya raia 270,000 na kuwaacha mamilioni ya wengine bila makaazi. Upinzani unasisitiza ni lazima Assad aondoke madarakani ili muafaka juu ya mzozo huo uweze kupatikana.

Syrien Präsident Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: imago/ITAR-TASS

Hata hivyo hatua ya kusimamisha mapigano kwa muda iliyoanza kutekelezwa mwezi uliyopita imetoa matumaini ya kumalizika mapigano hasa wakati Urusi, mshirika mkuu wa rais Assad ilipotangaza kuondoa majeshi yake yote nchini Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kuelekea Urusi kuijadili Syria.

Lakini hali ya wasiwasi imerejea tena baada ya Urusi kuishutumu Marekani kuchelewesha makubaliano ya namna ya kuwaadhibu wale watakaokiuka makubaliano ya kusitisha mapigano huku ikionya kuwa hilo linaweza kusababisha utumiaji nguvu dhidi ya wakiukaji wa makubaliano hayo. Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anatarajiwa kusafiri kuelekea Urusi kujadili hilo.

Kumekuwa na wasiwasi mwengine pia wa iwapo makubaliano yoyote ya mani yanaweza kufikiwa katika uwanja wa mapambano nchini Syria kufuatia wanamgambo wa Hezbolla kusema watabakia nchini Syria hadi watakapowashinda wanamgambo wa IS na kundi la kigaidi la al Qaeda tawi la Syria.

John Kerry IS Völkermord Washington USA
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: picture-alliance/AP Photo/S.Applewhite

"Yale yote yaliyosemwa kuhusu sisi kuondoka Syria ni uwongo mtupu, tulikwenda Syria kuisaidia nchi hiyo kutoanguka mikononi mwa Daesh yani ISna kundi la Al-Nusra Front, kama tuna wajibu wa kuwa huko tutaendelea kuwa huko," alisema kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah.

Mwandishi: Amina Abubakar /AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman