Mazungumzo ya Brexit kuanza Juni 19
23 Mei 2017Michel Barnier ambaye alichaguliwa bila kupingwa kuwa mpatanishi mkuu wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala la Brexit na kuamriwa kuuwakilisha umoja huo kuanzisha mazungumzo na Uingereza, amesema hatua ya nchi zote 27 wanachama kuunga mkono ni ishara nyingine inayoonyesha ari na ujasiri katika kipindi cha miaka miwili ya mazungumzo magumu kati ya pande hizo mbili.
Barnier ambaye ni kamishna wa zamani wa Umoja wa Ulaya na waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa pia amemuonya mwenzake wa Uingereza Davis Davis dhidi ya vitisho zaidi kujiondoa kwenye mazungumzo iwapo umoja huo utawasilisha muswada wa talaka wa gharama ya euro bilioni 100. Davis alirudia kitisho cha kuyagomea mazungumzo hayo iwapo Umoja wa Ulaya hautayafanyia marekebisho matakwa yake.
Akizungumza muda mfupi baada ya Umoja wa Ulaya kuridhia rasmi mpango wake kuhusu mazungumzo ya Brexit, Barnier alisema wako tayari. "Kutoka siku Uingereza ilipoamua kujitoa, tumefanya mchakato mkubwa wa maandalizi. Tuko tayari na tumejiandaa barabara. Tuna mamlaka wazi inayoungwa mkono na nchi zote 27 wanachama. Tuna azimio imara kutoka kwa bunge la Ulaya. Tuna mahusiano mazuri kikazi kati ya taasisi zote za Umoja wa Ulaya. Tuna timu ya wapatanishi. Miundo yote iko tayari."
Barnier amesema timu mpya ya Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit itakutana leo kukamilisha msimamamo wa mazungumzo ambao utatumwa haraka mjini London baada ya uchaguzi wa Juni 8 ambao waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anapania kuyaimarisha mamlaka yake. "Natumai kuandaa duru ya kwanza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo, pengine wiki ya Juni 19. Ningependa niweze kuwasilisha ripoti ya kwanza kwa baraza la Ulaya Juni 22 na 23."
Banier anatumai kuwaona wenzake wa Uingereza katika meza ya mazungumzo na anatarajia kukaribisha mazingira mazuri kutafuta msimamo wa pamoja.
Mshikamano ndani ya Umoja wa Ulaya
Naibu waziri mkuu wa Malta, Louis Grech, ambaye nchi yake inashikilia urais wa kuzunguka wa Umoja wa Ulaya, amesema uamuzi wa jana Jumatatu unaonyesha umoja na mshikamano unaendelezwa ndani ya kanda hiyo. "Utaratibu wa kwanza tutakaoufanya ni kuhusu Uingereza kujitoa. Utaratibu huu utafanyiwa marekebisho kadri mazungumzo yatakavyokuwa yakiendelea. Sasa kila kitu kiko sawa na mazungumzo yanaweza kuanza."
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, aliyechukua wadhifa huo kutoka kwa David Cameron kufuatia kura ya maoni ya Brexit Juni mwaka uliopita na kuanzisha mchakato wa kuitoa Uingereza kutoka kwa Umoja wa Ulaya Machi 29, alitoa muongozo kama huo wa kuanza kwa mazungumzo. "Siku 17 zimebaki kabla uchaguzi mkuu. Siku 11 baadaye Umoja wa Ulaya unataka mazungumzo ya Brexit yaanze," alisema May kwenye mkutano wa kampeni huko Wales. "Hakutakuwa na muda wa kupoteza wala muda kwa serikali mpya kutafuta njia yake," akaongeza kusema Bi May.
Umoja wa Ulaya unasisitiza umepiga hatua kuhusu masuala matatu muhimu kabla mazungumzo kuanza kuhusu mkataba wa biashara kati ya umoja huo na Uingereza. Masuala hayo yanajumuisha haki ya raia wa Umoja wa Ulaya wanaoshi Uingereza na raia wa Uingereza barani Ulaya, muswada wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya na mipango kuhusu mpaka kati ya Ireland na jimbo la Uingereza la Ireland Kaskazini. Uingereza inataka mazungumzo kuhusu Brexit na uhusiano wa baadaye yajadiliwe sambamba, lakini Umoja wa Ulaya umesema hapatafanyika mazungumzo kuhusu biasharaka kabla muswada wa Brexit kukamilika.
Mwandishi: Josephat Charo/afpe/rtre
Mhariri: Bruce Amani