Mazungumzo ya ana kwa ana yameanza
26 Januari 2014Wajumbe wa majadiliano kutoka upande wa serikali na upinzani walikabiliana katika meza ya majadiliano katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa muda wa karibu saa tatu pamoja na mpatanishi wa kimataifa Lakhdar Brahimi, ambaye ameueleza mkutano huo kuwa ni "mwanzo mzuri".
Wakati tofauti za kisiasa, ambazo Brahimi anasema zitajenga msingi wa mazungumzo yao zinaonekana kuwa kubwa mno kwa sasa, pande hizo mbili zimelenga jana Jumamosi kuhusu uwezekano wa makubaliano ya kiutu yenye lengo la kujenga hali ya kuaminiana katika hatua hizo za mazungumzo.
Brahimi amesema ana matumaini kuwa maafisa nchini Syria wataidhinisha hatua za kufungua njia leo Jumapili ili mlolongo wa magari yaliyochukua misaada kufika katika eneo linaloshikiliwa na waasi katikati ya Homs, na kuuruhusu kugawa misaada siku ya Jumatatu.
"Hatujapata mafanikio ya kutosha, lakini tunaendelea," amewaambia waandishi habari baada ya mazungumzo kukamilika kwa siku hiyo.
Wajumbe watenganishwa
Wakiwa na shauku ya kuepusha uwezekano wowote wa makabiliano, watayarishaji wa mkutano huo wamehakikisha kuwa pande hizo mbili ziliingia na kutoka katika chumba cha mkutano , katika mkutano wa asubuhi na mchana kwa kutumia milango tofauti.
Brahimi amesema kuwa walikabiliana wakati wa mkutano huo , lakini walitoa maelezo yao kupitia yeye.Hali ndivyo inavyokuwa katika majadiliano ya kistaarabu, unazungumza na rais ama na spika ama na mwenyekiti," amesema.
Mpatanishi huyo wa kimataifa mwenye uzoefu mkubwa , pia amesema kuwa ameweka mipango yake kwa ajili ya mazungumzo hayo katika muda wa wiki zijazo, akisisitiza kuwa ni lazima mazungumzo hayo yalenge katika utekelezaji wa maazimio ya Juni 2012 ambayo yanataka kuundwa kwa chombo cha uongozi cha muda kwa ridhaa ya makundi yanayopingana nchini Syria.
"Ametuambia kuwa huu ni mkutano wa kisiasa .....ulio chini ya msingi wa Geneva I," mjumbe wa upinzani Anas al-Abdah amesema, akizungumzia kuhusu makubaliano ya mwaka 2012 yaliyotangazwa na mataifa makubwa yenye nguvu duniani katika mji wa Uswisi ambako mazungumzo ya jumamosi yalifanyika.
Ujumbe wa serikali ya rais Bashar al-Assad umesema umekubali kwa kiasi kikubwa mkutano wa geneva I, lakini umerudia upinzani wake wa muda mrefu kuhusiana na wazo hilo la kuundwa kwa chombo cha uongozi wa mpito, na kusema ni kinyume na utaratibu na si lazima.
"Tuna dukuduku letu kuhusiana na makubaliano hayo," waziri wa habari Omran Zoabi amesema, akilinganisha pendekezo hilo na serikali ya mpito iliyoundwa nchini Iraq na majeshi ya uvamizi ya Marekani baada ya kuangushwa kwa utawala wa Saddam Hussein mwaka 2003.
"Syria ni taifa lenye taasisi," ameongeza. "Chombo cha utawala wa mpito ....kinatokea mahali ambapo taifa limevurugika, ama halina taasisi."
Wapiga kura ndio watakaoamua
Upande wa upinzani umesisitiza kuwa ujumbe wa serikali umekubali kimsingi kuunda chombo cha uongozi wa mpito, ukisema chombo hicho kitafikisha mwisho utawala wa Assad. Rais anasema ni wapiga kura tu wa Syria ambao wanaweza kuchangua utawala wao na kwamba anaweza kugombea tena katika uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika Juni mwaka huu.
Wakati pande hizo mbili zinakutana mjini Geneva , mapigano yanaendelea nchini Syria. Shirika la kuangalia haki za binadamu limeripoti mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali ya rais Assad kusini mwa mji mkuu Damascus na mashambulio kadha ya jeshi la anga nchini humo, hususan katika eneo la kaskazini la Aleppo na vitongoji vya mji wa Damascus.
Helikopta zimefanya mashambulizi kadha ya mabomu ya mapipa dhidi ya kitongoji cha Daraya, limesema shirika hilo lenye makao yake nchini Uingereza limesema, na mapigano baina ya waasi pia yameendelea katika majimbo ya hassakeh na Aleppo.
Brahimi amesema mipango kwa ajili ya misaada mjini Homs, ambako wapiganaji wamezingirwa na majeshi ya Assad, imejadiliwa na maafisa wa Umoja wa mataifa na gavana wa mji huo na mahitaji yanaweza kufikishwa katika mji huo katika muda wa saa 24 baada ya kupatikana idhini kutoka serikalini mjini Damascus.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Bruce Amani