1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Syria yakaribia kuvunjika

15 Februari 2014

Hatua za amani nchini Syria ambazo zinalegalega zimefikia hatua za mkwamo kamili jna Ijumaa(14.02.2014) huku kukiwa na wasi wasi wa kuvunjika kabisa licha ya mbinyo wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/1B9bs
Syrien-Gespräche UN Genf
Mkutano kati ya serikali na upinzani nchini Syria unaofanyika mjini GenevaPicha: DW/C. Witte

Wakati huo huo nchini Syria kwenyewe idadi ya vifo inaongezeka.

Katika siku ya mwisho ya duru hii ya mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa , pande zinazopigana nchini Syria zinaonekana kuwa mbali katika mtazamo wao kuliko wakati wowote ule, wakikubaliana tu katika suala moja, ambalo ni kwamba mazungumzo hayo hayaelekei kokote.

"Tunasikitika sana kwamba duru hii ya mazungumzo haijapiga hatua," amesema naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Syria Faisal Muqdad, baada ya kukutana na mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi.

Lakhdar Brahimi Syrien-Gespräche UN Genf
Mpatanishi wa kimataifa Lakhdar BrahimiPicha: FABRICE COFFRINI/AFP/Getty Images

Kwa upande wao, msemaji wa upinzani Louay Safi amelalamika juu ya kushindwa kwa serikali kuonesha ushirikiano, na kukiri kuwa " mazungumzo yamefikia hatua ya mkwamo."

Duru ya mwisho

Umoja wa Mataifa umetangaza siku ya Ijumaa kuwa Brahimi amezialika pande hizo mbili kurejea katika meza ya majadiliano kwa ajili ya duru ya mwisho ya mkutano wao wa pamoja leo Jumamosi asubuhi.

Wakati pande hizo zimeshindwa kupata makubaliano mjini Geneva hata katika ajenda zilizopo katika mazungumzo yao, idadi ya vifo ndani ya Syria inaendelea kupanda.

Schweiz Syrien Konferenz in Genf Louay Safi
Msemaji wa upinzani Louay al-SafiPicha: Getty Images/AFP/Fabrice Coffrini

Kundi linaloangalia hali nchini humo limesema siku ya Alhamis zaidi ya watu 5,000 wameuwawa tangu duru ya kwanza ya mazungumzo kuanza Januari 22.

Kiasi ya watu 47 wameuwawa siku ya Ijumaa katika shambulio la bomu lililotegwa katika gari mbele ya msikiti kusini mwa kijiji kinachodhibitiwa na waasi cha Yaduda, wakati kundi linalopambana kwa nadharia ya jihad la ISIL limewauwa watu 27 wakati waasi hasimu wakiwafukuza kutoka katika vijiji katika jimbo la kaskazini la Aleppo.

Na Umoja wa Mataifa umeonya siku ya Ijumaa kuwa zaidi ya wakimbizi 2,700 walimiminika katika mpaka na Lebanon wakati shambulizi la majeshi ya serikali ya syria katika milima ya Qalemun likiendelea , na kusababisha hali ya tahadhari hususan kwa upande wa mji unaoshikiliwa na upinzani wa Yabrud , ukitarajia kushambuliwa na jeshi la aridhini la Syria.

Vifo zaidi

Maelfu ya watu tayari wameukimbia mji huo , lakini zaidi ya watu 50,000 wanaaminika kuwa bado wako katika mji huo. Marekani imeeleza kukasirishwa kwake kutokana na shambulio la anga na kuzingirwa kwa mji huo.

"Tunatoa wito tena kwa jumuiya ya kimataifa , ikiwa ni pamoja na washirika wa Assad, kuueleza utawala huo kwamba ni lazima usitishe mashambulizi haya yasiyo lazima ambayo yanavuruga hatua za mazungumzo ya Geneva na matumaini ya amani nchini Syria," msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Edgar Casquez amesema.

Mjini Geneva kulikuwa hakuna ishara ya hatua za maendeleo kuelekea kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka mitatu sasa na kuuwa zaidi ya watu 136,000 na kuwalazimisha mamilioni wengine kukimbia nchi hiyo na wengine kukimbia makaazi yao.

Haifahamiki iwapo Brahimi ataweza kuzishawishi pande zinazohusika kurejea tena kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo.

Marekani , ambayo inaunga mkono upinzani na ambayo imeshawishi kuitishwa kile kinachofahamika kama Geneva II pamoja na Urusi ambayo ni mshirika wa utawala wa Syria , imeeleza fadhaa yake kutokana na kukwama kwa mazungumzo hayo.

Sergei Lavrov Russland Porträt
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi sergei LavrovPicha: Reuters

"Mazungumzo kwa ajili ya kujionesha tu hayana maana," Amsema afisa mwandamizi wa Marekani siku ya Ijumaa.

Katika juhudi za kuweka uhai katika mazungumzo hayo, Marekani na Urusi zimetuma wajumbe wa ngazi ya juu katika mazungumzo hayo ya Geneva wiki hii kukutana na Brahimi pamoja na pande hizo mbili.

Lakini baada ya kukutana na wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani na Urusi siku ya Alhamis, mpatanishi huyo amekiri kuwa " hali ya kushindwa bado inatukodolea macho".

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Sudi mnette