1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Syria yaendelea Geneva

Mjahida 17 Machi 2016

Mazungumzo ya amani ya kumaliza mgogoro wa Syria yametanuka kwa kuwajumuisha wapinzani waliokaribu na Urusi, wakati Umoja wa Mataifa ukizidisha juhudi za kutafuta suluhu ya kisiasa katika mzozo huo.

https://p.dw.com/p/1IEWI
Syrien UN-Vertreter Bashar Jaafari
Mkuu wa ujumbe wa serikali ya Syria Bashar al-JaafariPicha: picture alliance / AA

Kwa mara ya kwanza mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Syria Staffan de Mistura alikutana na ujumbe unaojulikana kama kundi la Moscow linalodai uwepo wa usawa katika meza ya majadiliano. Ujio wa kundi hilo unaonekena kupingwa na upinzani rasmi ambao ni kamati kuu ya upinzani HNC wanaosisitiza kuwa wao pekee ndio wanaopaswa kuuwasilisha upinzani wa Syria katika mazungumzo hayo.

Hata hivyo serikali ya Syria imesema haitoingia katika majadiliano na kamati kuu ya upinzani wanaoungwa mkono na Saudi Arabia, kwa kuwa hawawakilishi pande zote za upinzani nchini humo. Mkuu wa ujumbe wa serikali ya Syria Bashar al-Jaafari ametoa matamshi hayo baada ya kufanya mazungumzo ya saa mbili na staffan di Mistura.

"Hakuna mtu anayeweza kuudhibiti upinzani, hatuwezi kuwa na mazungumzo na kundi moja pekee lakini tunataka kuwa na mazungumzo na wajumbe wote wa upinzani, kama ujumbe wa serikali ya Syria, hatutaki kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na magaidi, wajumbe wanaoungwa mkono na Saudi Arabia ni magaidi "alisema Bashar al Jaffari.

Schweiz Syrien-Friedensgespräche in Genf
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Syria Staffan de MisturaPicha: Reuters/R. Sprich

Wakati huo huo Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema huenda kukakosekana nafasi ya kipekee ya kumaliza mapigano Syria iwapo mazungumzo hayo yataanza kuingia doa.

Urusi yasema itaondoa vikosi vyake vyote Syria siku mbili au tatu zijazo.

Kwa upande wake Umoja wa Mataifa haukuweka wazi jukumu litakalopewa kundi hilo la Moscow katika mazungumzo hayo. Kuingia katika mazungumzo hayo ya Geneva kundi hilo la Moscow pamoja na na kundi la Cairo na Istana ilitokana na hatua ya kushtukiza ya Urusi ya kuondoa baadhi ya vikosi vyake nchini Syria, ambapo vilikuwa vikipigana kwa kumuunga mkono rais Bashar al Assad.

Aidha serikali za mataifa ya Magharibi zimesema Urusi kuendelea kuondoa vikosi vyake nchini Syria, huenda kukatoa matumaini ya kupatikana muafaka katika mazungumzo ya amani kwa kutoa shinikizo kwa rais Assad.

Syrien Abzug russischer Militärflugzeuge
Ndege za kivita za Urusi zikirejea nyumbani kutoka Syria.Picha: picture-alliance/dpa/Russian Defense Ministry

Urusi inasema mashambulizi yake ya miezi mitano nchini Syria yamesaidia kuwasukuma kando makundi ya jihadi huku wachambuzi wakisema hatua hiyo imesaidia vikosi vya Assad na kuwasaidia kudhibiti maeneo muhimu nchini humo.

Kulingana na kamanda wa jeshi la angani la Urusi Viktor Bondarev amesema nchi hiyo itakamilisha operesheni ya kuondoa vikosi vyake vyote nchini Syria katika siku mbili au tatu zijazo.

Tangu mgogoro uanze nchini Syria miaka mitano iliyopita, watu 270,000 wameuwawa huku mamilioni ya wengine wakiachwa bila makao wengi wakitafuta maisha mapya ulaya ambapo ongezeko la wakimbizi na wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati, Afrika na Asia ikisababisha changamoto kubwa kwa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Yusuf Saumu