1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Syria yaanza Astana

23 Januari 2017

Mkutano wa kuutafutia ufumbuzi wa mgogoro wa Syria umefunguliwa leo katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana ambapo wawakilishi wa makundi ya waasi wanakutana na upande wa serikali.

https://p.dw.com/p/2WEgT
Kasachstan Syrien Friedensgespräche in Astana Opposition
Picha: Reuters/M. Kholdorbekov

Mazungumzo hayo yamekaribishwa na pande zote katika vita hivyo, lakini pande zote mbili ziliwasili nchini Kazakhstan zikiwa na mawazo tofauti kuhusu lengo lao, na maafisa wametilia shaka kama kweli wataweza kukaa meza moja.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kazakhstan Karait Abdrakhmanov ameyafungua mazungumzo hayo ambapo aliwaambia wajumbe wa serikali na waasi waliokaa pamoja kwenye meza ya duara kuwa ni jukumu la wahusika wote kupata ufumbuzi ambao utawafaa Wasyria. "tumejitolea kutoa msaada kwa wenzetu, wadhamini wa mkutano huu na kwa Umoja wa Mataifa pamoja na serikali ya Syria na makundi ya upinzani yenye silaha. tunawathamini sana na kuwashukuru kwa kushiriki na kwa kazi kubwa itakayofuata".

Syrien  UNO-Gesandter für Syrien Staffan de Mistura in Damaskus
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de MisturaPicha: AFP/Getty Images/L. Beshara

Hata hivyo, Muungano wa Kitaifa wa Upinzani nchini Syria umesema mazungumzo halisi hayatakuwa ya ana kwa ana kwa sababu muda haujafika.

Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Kazakhstan Roman Vasilenko aliwaambia wanahabari mapema leo kuwa muundo wa mazungumzo hayo bado unajadiliwa.

Makundi ya waasi yanasema mkutano huo utaangazia katika kuimarisha mpango tete wa usitishwaji mapigano kote nchini Syria uliofikiwa mwezi uliopita kati ya mshirika wa upinzani Uturuki na Urusi inayoiunga mkono serikali. Yahya Al Aridi ni msemaji wa upinzani "Kuna maswala mawili ya kujadiliwa. kwanza uimarishaji wa mpango wa kusitisha mapigano uliofikiwa na Uturuki na Urusi na kuufanya mpango huo kutekelezwa kote Syria na kuzungumzia ukiukaji unaofanywa na serikali na Iran. Kama hilo litafanikiwa, huenda ikasaidia katika mchakato wa kisiasa".

Lakini Assad anasisitiza kuwa waasi waweke chini silaha zao ili nao wasamehewe, na kutoa wito wa kuwapo suluhisho pana la kisiasa kwa mgogoro huo uliowauwa zaidi ya watu 310,000 na kuwaacha wengine zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Syria bila makaazi.

Kasachstan Syrien Friedensgespräche in Astana
Wajumbe wa serikali na wa upinzani hawatajadiliana ana kwa anaPicha: Reuters/M. Kholdorbekov

Huku yakiandaliwa na Uturuki, Urusi na Iran, mazungumzo hayo yanakuja mwezi mmoja baada ya serikali kuyakomboa maeneo ya waasi mjinji Aleppo, ikiwa ni ushindi mkubwa tangu vita hivyo vilipoanza.

Juhudi za  awali za kufikia mpango wa kudumu wa kusitisha mapigano nchini Syria zimevurugwa, huku pande zote zikinyosheana kidole cha lawama. Wajumbe 10 wa serikali, wakiongozwa na balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar al-Jaafari pia wanahudhuria mazungumzo hayo.

Malengo ya serikali pia ni pamoja na kufikia "msimamo wa pamoja” na washiriki wengine. Serikali imekutana leo na ujumbe wa Iran, pamoja na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura kabla ya mazungumzo ili kujadili misimamo yao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri : Gakuba, Daniel