Mazungumzo ya amani ya Syria kuanza tena Geneva
22 Februari 2017Baada ya miezi kumi ya mkwamo wa mazungumzo ya amani ya Syria, juhudi hizo zinaanza upya Alhamisi. Hata hivyo inahofiwa huenda mambo yaliyochangia kusababisha mkwamo huo yakajitokeza tena, licha ya kuwepo kwa mabadiliko makubwa katika muktadha wa kijeshi na kisiasa.
Wawakilishi wanaoshiriki katika mazungumzo ya amani ya kumaliza vita nchini Syria wameanza kuwasili Geneva kuanza mazungumzo hayo kesho. Hata hivyo upinzani umedai kuwa kufuatia operesheni za kijeshi zinazofanywa, serikali ya Syria na washirika wake wanajaribu kuhujumu mazungumzo hayo. Madai yanayoashiria hali ya kutoaminiana kati ya pande mbili husika kwenye mazungumzo hayo.
Akiwa mjini Geneva kabla ya mazungumzo kuanza, msemaji wa upinzani Ahmed Ramadan amesema hali ni kama ile ile ya mwaka jana ambayo iliwalazimu wapinzani kujiondoa wakilalamikia kuendelea kwa mashambulio ya vikosi vya Syria na washirika wake. Haya yanajiri wakati Jeshi la Syria na washirika wake likiwa limechukua udhibiti wa wilaya ndogo iliyoko nje ya Aleppo kutoka mikono ya waasi.
Mwakilishi wa upinzani katika mazungumzo hayo Ahmad Ramadan amesema lengo lao kuu ni uongozi wa mpito "Ujumbe wa upinzani utalenga mchakato wa mpito wa kisiasa. Tunachukua kuanza kwa mazungumzo haya kuwa hatua muhimu hasa ikizingatiwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura wamethibitisha mazungumzo yatalenga utawala wa mpito, mikakati ya kuundwa kwake, katiba na uchaguzi."
Ajenda ambazo zimeundwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadiliwa kwenye mazungumzo hayo zinalenga mpango wa utawala wa mpito kati ya serikali na upinzani, katiba mpya na uchaguzi. Hizi zote zikiwa juhudi za kujaribu kumaliza vita ambavyo vimedumu kwa miaka sita sasa.
Masuala yenye utata
Tangu Aprili mwaka uliopita, wakati mazungumzo hayo ya amani yalipovunjika, vikosi vya Rais Bashar al-Assad kwa ushirikiano na majeshi ya Urusi na Iran vimebadilisha hali. Kumekuwa na hatua chache sana ambazo zimefanywa kusuluhisha masuala yaliyogubika mazungumzo ya awali.
Upinzani utashinikiza kuachiliwa huru kwa wafungwa, kutaka serikali kuondoa marufuku na zaidi ya mno, kuwepo uongozi wa mpito utakaomaliza utawala wa Assad. Lakini Damascus inasisitiza kuwa hatma ya rais haipaswi kujadiliwa. Serikali inatarajiwa kushikilia mtizamo wake kuwa upinzani ambao umejihami ni magaidi.
Tangu mazungumzo hayo ya mwisho, serikali imedhibiti maeneo mengi ambayo awali yalikuwa ngome za upinzani ikiwemo mashariki mwa Aleppo
Hadi tukienda hewani, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura alitarajiwa kutoa hotuba kuhusu mazungumzo hayo.
Mwandishi: John Juma/RTRE/DPAE/AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu