Mazungumzo ya amani Syria yangali mashakani
3 Februari 2016Hayo ni wakati Urusi ikiapa kuwa haitasitisha mashambulizi yake ya angani katika hatua ya kuunga mkono utawala wa Rais Bashar al-Assad.
Juhudi za kubwa kabisa kufikia sasa za kujaribu kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria zilitumbukia katika mkanganyiko hapo jana baada ya upinzani kuufuta mkutano wake na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura katika hatua ya kukasirishwa na mamia ya mashambulizi ya angani yaliyofanywa na Urusi tangu Jumatatu.
Wawakilishi wa serikali ya Rais Bashar al-Assad waliikemea Kamati Kuu ya Majadiliano – HNC ambalo ndilo kundi kuu la upinzani, wakisema halina mwelekeo na lililojaa magaidi, wakati likitofautiana na de Mistura kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja tayari yameanza.
Upande wa upinzani unamtaka Assad kuruhusu uingizaji wa misaada ya kiutu katika miji iliyozingirwa, kukomesha mashambulizi ya mabomu dhidi ya raia na kuwaachia maelfu ya wafungwa – wengine wao watoto – wanaoendelea kuteseka katika magereza ya serikali.
Serikali ya Syria inasema upinzani umeshindwa kuwasilisha hata orodha ya wajumbe wake na inapinga vikali kujumuishwa kwa waasi ambao wanaonekana kuwa ni magaidi.
Mmoja wa viongozi kama hao ni Mohammed Alloush, mwanachama mkuu wa kundi la waasi la Jeshi la Kiislamu, ambaye amekuwa Geneva tangu Jumatatu na kawaida huwa mjumbe mkuu wa upinzani ambaye amesema leo kuwa “hana matumaini” kuhusu mazungumzo hayo.
Naye mkuu wa ujumbe wa serikali katika mazungumzo hayo Bashar al-Ja'afari amesema awamu ya maandalizi ya mazungumzo hayo ya Geneva huenda ikachukua muda mrefu zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
De mistura amesema ikiwa mazungumzo haya yatakwama, “matumaini yote yatakuwa yamepotea”. Kiwango cha uaminifu kinakaribia sifuri baina ya pande zote mbili. Kiwango cha uhasama baina ya pande zote ni kikubwa mno. Na hisia ya uharaka ambayo sote tunaihisi, pia ipo nao kwa sababu wanafahamu kuwa mzozo huu umedumu muda mrefu. Hivyo tulipo kwa sasa ni katika hatua ya maandalizi kwa ajili ya mazungumzo halisi.
Aidha amesema kuwa “kiwango cha matumaini baina ya pande mbili zinazoshiriki katika mazungumzo kinakaribia sifuri”.
Mashambulizi ya karibuni ya Urusi tangu nchi hiyo ilipotangaza kumuunga mkono kijeshi rais Assad mwishoni mwa mwezi Septemba yaliwaruhusu wanajeshi watiifu kukaribia kuvunja vizuizi vilivyowekwa na waasi katika vijiji viwili vinavyodhibitiwa na serikali karibu na mji wa Aleppo.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema leo kuwa haoni haja yoyote ya kusitishwa mashambulizi ya angani, huku akiwashutumu magaidi katika upande wa upinzani na kile alisema ni uingizaji silaha Syria kutokea Uturuki.
Mwandishi: Bruce Amani/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef