May akabiliwa na kura ya kutokuwa na imani
12 Desemba 2018Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn, walirushiana maneno makali bungeni siku ya Jumatano (Novemba 12), wakati wa mjadala mkali uliotangulia kura imani kwa uongozi wa May kutokana na namna alivyoliendesha suala la makubaliano ya nchi yake kujiondoa Umoja wa Ulaya, Brexit.
"Corbyn anapaswa kuwa mkweli kwa watu juu ya msimamo wake. Hajali chochote kuhusu Brexit, isipokuwa anachotaka ni kuiangusha serikali, kutengeneza hali ya ukosefu wa imani, migawanyiko na kuuharibu uchumi wetu. Kitisho kikubwa kwa watu na nchi hii sio Brexit, bali ni Cobin na Labour yake," alisema May kwa sauti ya hasira.
Mdahalo huu ulitajwa na wachambuzi wa siasa za Uingereza kwamba ulikuwa mkali zaidi baina ya May na Corbyn kuwahi kushuhudiwa kwa siku za karibuni.
Wakati May akimtuhumu Corbyn kutaka kuiangusha serikali yake na kuleta machafuko ya kijamii na kiuchumi, Corbyn ameliambia bunge kuwa May hapaswi kuendelea na wadhifa wake kutokana na kuliendea kinyume bunge hilo na watu wa Uingereza.
"Mheshimiwa Spika, tabia chafu ya waziri mkuu lazima ichukuliwe hatua. Bunge hili na watu wa nchi hii wanazidi kutiwa mashaka na machafuko yaliyomo kwenye serikali yake mwenyewe."
Mdahalo huu ulitangulia kura ya imani bungeni iliyotazamiwa kupigwa baina ya saa 12:00 jioni na 2:00 usiku kwa majira ya London.
Wabunge 158 wamuunga mkono May
Hata hivyo, tayari wabunge 158 wa chama cha May, Conservative, wameshatangaza hadharani kuwa wanamuunga mkono kiongozi wao huyo, kwa mujibu wa taarifa walizoziatangaza kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
May anahitaji kupata wingi mdogo wa kura 158 kati ya 315 kuweza kuendelea na wadhifa wake wa waziri mkuu, ambapo kama atashinda, basi sheria inazuwia uwezekano wa kuitisha kura ya kutokuwa na imani naye kwa kipindi cha miezi sita ijayo.
Uingereza inatakiwa iwe imeshajiondoa rasmi kwenye Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi Machi mwakani.
Haya yakijiri, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya unaoanza Alhamis (Novemba 13) usingelikuwa na matokeo yoyote kwenye mabadiliko ya makubaliano kujiondoa kati ya Umoja huo na Waziri Mkuu May.
"Hatuna dhamira ya kubadilisha makubaliano ya Brexit tena, na huo ndio msimamo wa pamoja wa mataifa 27 wanachama," Kansela Merkel aliliambia bunge mjini Berlin, akiongeza kwamba isitarajiwe baada ya majadiliano ya kesho Alhamis na keshokutwa Ijumaa, Umoja wa Ulaya utatoka na mabadiliko yoyote.
May alitazamiwa kuwaeleza viongozi wenzake wa mataifa ya Ulaya juu ya yanayojiri kwenye makubaliano hayo hapo kesho mjini Brussels. Alikuwa kwenye ziara ya ghafla hapo jana kwenye mataifa matatu akisaka hakikisho la kumsaidia kuyawasilisha makubaliano yake na Umoja wa Ulaya mbele ya bunge.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga