May akabiliana na mpinzani wake Corbyn
30 Mei 2017Wawili hao walikabiliwa na mdahalo wa moja kwa moja wa Televisheni usiku wa jana Jumatatu, kuelekea uchaguzi mkuu mwezi ujao.
Siku kumi kabla ya uchaguzi wa mapema wa Juni 8, mahasimu hao wawili kila mmoja kwa wakati wake walikabiliwa na maswali kadhaa kutoka kwenye hadhara ya waliohudhuria kabla ya kuhojiwa na mtangazaji mkongwe Jeremy Paxman.
May alikataa mdahalo wa ana kwa ana na Corbyn, ambaye chama chake cha upinzani katika siku za hivi karibuni kimepunguza pengo lake kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya wapiga kura, ingawa chama tawala cha Conservative bado kimesalia nafasi ya usoni.
Wakati Corbyn alisisitiza kwamba "angehakikisha kunakuwa na makubaliano" na Umoja wa Ulaya kabla ya Uingereza kujiondoa katika muungano huo, May alisema "amejiandaa kutoka nje".
Alivyoulizwa ikiwa anafahamu thamani ya kujiondoa umoja huo alisema kwamba, "si hoja ya thamani gani ya kujiondoa bali ni hoja ya yapi yatakuwa makubuliano sahihi kwetu kujiondoa Umoja wa Ulaya, ambayo itatusaidia sisi kuacha kulipa kiasi kikubwa cha pesa katika umoja huo kila mwaka."
Wagombea wote wawili walikuwa wanaunga mkono kubakia ndani ya Umoja wa ulaya kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni Juni 2016, ambapo asilimia 52 ya wapiga kura wa Uingereza walichagua kujitoa.
Mazungumzo rasmi ya Uingereza kujiondoa yanatarajiwa kuanza Juni 19, ikiwa ni siku 11 baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Pamoja na mammbo mengine pia mpinzani wake Corbyn aligusia namna ya kukabiliana na ugaidi na akasema kwamba, "nadhani kuna haja ya kuwa na kile ambacho ni muhimu ili kuokoa na kulinda maisha ya watu. Nataka kuishi katika jamii iliyo salama. Kimsingi hakuna mtu anataka kuona maafisa wa polisi walokuwa na silaha kila mahali. Ukweli ni kwamba kwa wakati huu wamekuwa na umuhimu mkubwa".
Mnamo mwezi Machi Bibi May alianzisha rasmi utaratibu wa kujiondoa Umoja wa Ulaya na kisha kuanzisha ratiba ya miaka miwili kwa ajili ya majadiliano kabla ya kujiondoa katika muungano huo.
Usalama ulikuwa pia ni sehemu ya ajenda katika mdahalo wa jana kufuatia shambulizi la kujitoa muhanga mjini Manchester wiki moja iliyopita ambapo watu 22 waliuawa na kupelekea kusimamishwa kwa muda kwa kampeni za kisiasa.
May, ambaye mara kadhaa alizomewa na hadhara iliokuwepo wakati wa mdahalo huo wa televisheni, aliulizwa na polisi mmoja kuhusu kupunguzwa kwa idadi kubwa ya askari polisi wakati wa utawala wake wa miaka sita kama waziri wa mambo ya ndani. Alijibu kwamba serikali iliyokuwepo ilitaka kuhakikisha Uingereza "inaishi kulingana na mapato yake" hasa kutokana na hali ya kiuchumi iliyoirithi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman