1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa NATO wakutana na kuahidi mshikamano na Ukraine

29 Novemba 2023

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Kujihami NATO wamekutana Jumatano mjini Brussels nchini Ubelgiji, ili kujadili hali halisi katika uwanja wa vita huko Ukraine pamoja na msaada wa mataifa ya Magharibi kwa taifa hilo

https://p.dw.com/p/4ZZN3
Belgien | NATO Ukraine Treffen
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock (mbele kushoto), Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba (katikati) na Jens Stoltenberg Katibu mkuu wa NATO wakiwa mjini Brussels katika mkutano huo: 29.11.2023Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Juhudi za Ukraine za kuboresha vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili kufikia viwango vinavyohitajika na NATO, ilikuwa pia miongoni mwa ajenda hasa kwa kuzingatia matarajio ya Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo.

Mawaziri hao wa mambo ya nje wanapaswa kufanya mijadala yao kwa mara ya kwanza katika Baraza lililo rasmi la NATO-Ukraine ambalo liliundwa hivi karibuni ili kuwezesha ushirikiano hadi Ukraine itakapokamilisha masharti ya uanachama.

Baraza hilo liliundwa mwezi Julai katika mkutano wa kilele wa  NATO huko Vilnius nchini Lithuania, wakati viongozi wa NATO walipokutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky. Tangu wakati huo, kumekuwa na mkutano mmoja katika ngazi ya mawaziri wa ulinzi na mikutano kadhaa ya mabalozi wa NATO.

Lettlands Außenminister Krisjanis Karins im DW-Interview
Waziri wa Mambo ya Nje wa Latvia, Krisjanis Karins akihojiwa na DWPicha: Lucia Schulten/DW

Naye, Waziri wa Mambo ya Nje wa Latvia, Krisjanis Karins, amesema alipokuwa akiwasili makao makuu ya muungano huo wa kijeshi kuwa wanachama wa NATO wanahitaji kuanza kushughulikia hatua madhubuti ili kuisaidia Ukraine katika mchakato huo, hii ikiwa ni pamoja na masuala ya kisheria, kijeshi, taratibu za uendeshaji, vifaa pamoja na mbinu stahiki.

Waziri Karins ameongeza kusema kuwa kwa sasa, hakuna haja ya kuanzisha mijadala ya lini na jinsi gani Ukraine itajiunga na NATO, lakini akasisitiza kuwa wanahitaji kuchukua hatua kwa vitendo.

Msimamo wa Ukraine kuhusu vita na uanachama katika NATO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema akiwa mjini Brussels leo hii kwamba kufikia sasa, Umoja wa Ulaya tayari umetoa takribani makombora 300,000 miongoni mwa mamilioni yaliyoahidiwa kwa Ukraine.

Akizungumza na waandishi habari pembezoni mwa mkutano huo, Kuleba ametoa wito wa uwiano zaidi katika sekta ya ulinzi kati ya Ukraine na NATO ili kuhakikisha Kyiv ina vifaa inavyovihitaji ili kuishinda Urusi, ambayo iliivamia Ukraine mnamo Februari 2022. Aidha, Kuleba amesema haiwezekani kuulinda Umoja wa Ulaya bila ya kuilinda Ukraine:

Belgien | NATO Ukraine Treffen
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO Jens Stoltenberg mjini Brussels, Ubelgiji: 29.11.2023Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

" Ushindi wa Ukraine sio kwa maslahi ya Ukraine pekee, bali jumuiya nzima ya NATO. Haitakuwa kuyazidisha mambo nikisema kwamba kutetea Ulaya bila Ukraine ni kazi bure. Huwezi kufanya hivyo, kwa sababu moja na rahisi kwamba, kwa sasa tuna jeshi lenye nguvu na lenye uwezo mkubwa zaidi wa kupambana barani Ulaya."

Soma pia: Wanachama wa NATO waahidi kuendelea kusimama na Ukraine

Kuleba amesisitiza pia Ukraine "haitarudi nyuma" katika mapambano yake dhidi ya Urusi, licha ya mashaka yaliyopo juu ya uungwaji mkono wa Marekani na mafanikio madogo kwenye mstari wa mbele wa vita. Amesema lengo la kimkakati la Ukraine ni kurejesha maeneo yake yaliyonyakuliwa kinyume cha sheria na Urusi ikiwa ni pamoja na Rasi ya Crimea.

Ama kuhusu suala la uungwaji mkono, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, amesema Washington na washirika wake wataendelea bila kutetereka kuiunga mkono Ukraine katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi. 

Baadhi ya maafisa wa mataifa ya Magharibi wamesema hawaishinikizi Kyiv kufanya mazungumzo na Moscow licha ya kauli ya hivi karibuni ya afisa mwandamizi katika jeshi la Ukraine kusema kuwa vita hivyo sasa vimesababisha mkwamo wa umwagaji damu.

Huku hayo yakijiri, mapambano yameendelea. Jeshi la Ukraine limesema hii leo kuwa limefanikiwa kudungua ndege 21 zisizo na rubani za Urusi huku, Moscow ikiripoti pia mashambulizi kama hayo katika ardhi yake.