1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa NATO wajadili msimamo wa pamoja kwa Urusi

7 Januari 2022

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanakutana mjini Brussels kukubaliana msimamo wa pamoja kwenye mazungumzo baina ya jumuiya hiyo na Urusi juu ya suala la Ukraine.

https://p.dw.com/p/45GV7
Ukraine Polen Litauen Präsidenten
Picha: Konstantin Sazonchik/TASS/dpa/picture alliance

Miongoni mwa ajenda muhimu za mkutano huo wa leo ni matayarisho ya mataifa wanachama wa NATO kwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi endapo Moscow itaingia kijeshi nchini Ukraine ama mipango ya kitaifa kuongeza usambazaji silaha kwa Ukraine.

Mkutano huo kwenye makao makuu ya NATO mjini Brussels unalenga hasa kuufanya umoja huo wa kijeshi kuwa na mkakati mmoja mahasusi, huku wawakilishi kutoka NATO na Urusi wakitazamiwa kukutana Jumatano ijayo katika mji mkuu huo wa Ubelgiji.

Wasiwasi unazidi kuongezeka katika mataifa ya Magharibi kwamba Urusi inaweza ikaanzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Ukraibe kama ilivyotokea mwaka 2014, pale Moscow ilipolitwaa jimbo la Crimea na kuanza kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.

Urusi inakataa shutuma dhidi yake kwamba inajitayarisha kwa uvamizi huo wa kijeshi, na badala yake inaituhumu Ukraine kwa kupeleka vikosi vyake kuelekea mkoa wa Donbas ambao unadhibitiwa na waasi wanaoiunga mkono Urusi.

Lettland NATO Militärübeung Winter Shield
Urusi haitaki NATO ijitanuwe zaidi kuelekea mashariki mwa Ulaya.Picha: Gints Ivuskans/Getty Images/AFP

Rais Vladimir Putin wa Urusi anataka pia NATO itamke wazi kwamba haitaendelea kujitanuwa kwenye mataifa ya mashariki mwa Ulaya, ikiwemo ahadi ya kutokuipa uwanachama Ukraine.

Urusi inasema inahisi usalama wake unatishiwa jinsi NATO inavyosonga mbele, lakini Sweden imesema hivi leo kwamba usalama wake utakuwa umehujumiwa moja kwa moja ikiwa NATO itakuballiana na wazo la Urusi la kujizuwia kujitanuwa na kupunguza harakati zake barani Ulaya.

Sweden yahofia usalama wake

Sweden si mwanachama wa NATO na haina mpango wa kujiunga na Umoja wa huo lakini ina ushirikiano wa karibu na maalum na jumuiya hiyo ya kijeshi.

Muungano huo wa kijeshi wa mataifa ya Magharibi imepuuzilia mbali wazo kwamba imekuwa kitisho kwa Moscow, ikisema madai hayo ni ya ovyo. 

Suala hilo litajadiliwa kwenye mkutano wa wiki ijayo, amabo ni sehemu ya mfululizo wa juhudi za kimataifa kuukwamua mzozo unaoendelea sasa, kabla ya kugeuka kuwa mbaya zaidi.

Wanadiplomasia wa Urusi na Marekani pia wamepangiwa kukutana mjini Geneva siku za Jumatatu na Jumanne wiki ijayo. 

Hadi saa, zaidi ya watu 13,000 wameshauawa kwenye mzozo wa mashariki mwa Ukraine, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.